Mkuu wa sehemu ya Utangazaji Utalii wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Anna Lawuo(kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vivutio mbalimbali vinavyopatikana kwenye hifadhi zinazosimamiwa na Wakala huo .Kulia ni Mhifadhi Mwandamizi wa TFS katika Shamba la Miti West Kilimanjaro Robert Faida


 WAKALA wa Huduma za  Misitu Tanzania (TFS) kupitia Shamba la Miti la West Kilimanjaro wameandaa mashindano ya michezo ya pikipiki, baiskeli pamoja na mbio za marathon zinazotarajia kufanyika Juni 24 na 25, mwaka 2023 ambazo zitafanyika katika  Misitu hiyo.

Akizungumza leo Juni 14, 2023 jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari kuelekea West Kili Tour Challenge 2023 ,  Mratibu wa mashindano hayo Mensieut Elly amefafanua kutakuwa na michezo ya watoto na watu wazima  watakaokimbia mbio za marathon za km tano, 10 na 21.

Pia amesema kutakuwa na waendesha pikipiki watakaoendesha km 35 mpaka 75 wakipita kwenye kingo za Mlima Kilimanjaro sambamba na matembezi ya kuona maporomoko ya maji, mapango, ambapo litawahusisha wanamichezo na watu wa kawaida wanaotaka kwenda kutembelea na kula nyama choma.

"Gharama za ushiriki wa challenge hizi ni Sh 10,000 kwa watu wa kawaida wanaotaka kwenda kutembea na kula, sh 15,000 watakaoenda kwenye maporomoko na sh 35,000 kwa wanaotaka kushiriki mbio za marathon ambapo watapata medali na kila kitu.Mashindano yatashirikisha wageni kutoka Canada, Marekani, Kenya, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Tanzania, " amesema.

Awali Mhifadhi Mwandamizi wa TFS  Shamba la miti west Kilimanjaro Robert Faida amesema michezo hiyo imeandaliwa ikiwa ni sehemu mojawapo ya kutekeleza maelekezo ya Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa ya kuhimiza umuhimu wa kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii.

Ameongeza kupitia kampeni ya 'West kili Tour Challenge' itahusisha michezo mbalimbali huku akitumia nafasi hiyo kuihimiza jamii kushiriki kikamilifu kwenye ualii wa ndani kwa kutembelea vivutio, kutengeneza mitandao na watu wa Kimataifa pamoja na kufanya uwekezaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu ya Utangazaji Utalii TFS Anna Lawuo ameeleza kwamba  kuna misitu 23 ya kupandwa inayotumika kufanya michezo ya aina mbalimbali ikiwemo ya mbio za magari ambayo ina vigezo vya kitaifa na Kimataifa.

"Katika msitu huo kuna changamoto ya hotel hivyo, ni fursa kwa Watanzania kwenda kwenye michezo hiyo kuangalia maeneo yanayofaa kwa uwekezaji wa hoteli, " amesema.

Mratibu wa mashindano ya Marathon West Kili Tour Challenge 2023 Mensieut Elly akiwa kwenye kikao na waandishi wa habari wakati akielezea maandalizi ya mashindano hayo yanayotarajia kufanyika Juni 24 na Juni 25 mwaka huu katika Shamba la Miti West Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro
Share To:

Post A Comment: