Katibu Tawala Mkoa wa Singida (RAS) Dk. Fatuma Mganga akizungumza kwenye kikao kazi kilichofanyika Juni 23, 2023 cha wadau wa elimu cha kuweka mikakati ya kimkoa ya kuwalinda watoto shuleni dhidi ya vitendo vya ukatili. 

Na Dotto Mwaibale, Singida

KATIBU Tawala Mkoa wa Singida (RAS) Dk. Fatuma Mganga ameagiza kufungwa kwa kamera za usalama (CCTv Camera) katika shule ili kukomesha vitendo vya ukatili kwa watoto.

Dk.Mganga ametoa maagizo haya Juni, 23, 2023 wakati akizungumza kwenye kikao kazi cha wadau wa elimu cha kuweka mikakati ya kimkoa ya kuwalinda watoto shuleni dhidi ya vitendo vya ukatili.

"Matumizi ya teknolojia za kamera za usalama katika shule zetu zikiwekwa katika kila kona na kwenye magari ya kuwabeba wanafunzi zitasaidia kuonesha vitendo hivyo na kupata ushahidi wa moja kwa moja na kutokomeza ukatili wa aina zote hasa kwa watoto," alisema Mganga.

Aidha, Dk.Mganga aliomba kuanzishwa kwa madawati ya ulinzi na usalama kwa mtoto mashuleni jambo litakalo wafanya kuondoa woga wa kutoa taarifa za ukatili.

"Niwaagize maafisa elimu wote kuhakikisha shule zote zinakuwa na madawati ya ulinzi na usalama ili watoto waweze kujadili masuala ya ukatili na kutoa taarifa," alisema.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza sana kwenye miundombinu ya elimu ili kumsaidia mtoto wa kitanzania kupata elimu bure na bora hivyo ni jukumu la watendaji kusimamia watoto wasifanyiwe vitendo hivyo vya udhalilishaji.

Katika hatua nyingine Dk.Mganga alitoa rai kwa viongozi wa sekta ya elimu mkoani hapa katika shule zote za msingi na sekondari watoto wafundishwe kupitia wimbo wa 'Don't Touch kampeni' ulioasisiwa na Mkaguzi wa Polisi, Francis Msuku wa Kata ya Gambushi, Bariadi mkoani Simiyu na kupongezwa na Rais Samia ili waelewe jinsi ya kuzuia ukatili dhidi yao.

Ili kukabiliana na vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto na kufikia malengo yanayohitajika Dk. Mganga aliwataka maafisa ustawi na maendeleo ya jamii  kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi kutoa elimu kuhusu haki na wajibu wao katika kumlinda mtoto na kuwaelekeza vizuri ni wapi pa kukimbilia ili kupata huduma zinazostahili.

Pia Dk. Mganga aliagiza urasimu katika utoaji huduma uondolewe kabisa ili kuleta imani kwa wananchi kuhusu vyombo vyao vya dola.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick alisema jitihada mbalimbali zimeendelea kufanyika kwa kushirikiana na  wadau na wataalam wa maendeleo kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari na kutoa huduma za afya, unasihi,kisheria kwawahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

Dk. Mganga akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.
Wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, maafisa ustawi na maendeleo ya jamii, Polisi, walimu wakiwa kwenye kikao hicho.
Kikao hicho kikiendelea.
Taswira ya kikao hicho.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: