Na. Damian Kunambi, Njombe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa wilaya ya Ludewa kujipanga kwa kuzitumia fursa mabalimbali ikiwemo kupata ajira katika  miradi mikubwa ya Liganga na Mchuchuma ambayo mchakato wa utekelezaji wake unatarajiwa kufanyika mara baada ya kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha miradi hiyo.

Dkt. Samia amezungumza hayo kwa njia ya simu katika hafla ya uzinduzi wa malipo ya fidia kwa wananchi hao wanaopisha miradi ambayo imehudhuliwa na viongozi mabalimbali wa serikali, wabunge wa mkoa wa Njombe akiwemo mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga pamoja na  wananchi wanaolipwa fidia huku mgeni rasmi wa hafla hiyo akiwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ashatu Kijaji.

"Nilikuja Ludewa katika kipindi cha Kampeni nikiwa makamu wa Rais na niliahidi kushughulikia jambo hili la fidia lakini pia uanzishwaji wa miradi hii, na sasa nimetekeleza jambo hili kama nilivyoahidi". Amesema Dkt. Samia.

Alisema miradi hiyo itakapoanzishwa itatoa ajira nyingi kwa vijana pamoja na fursa za kibiashara huku mapato ya Halmashauri ya Ludewa, mkoa na nchi kwa ujumla yataongezeka hivyo ni vyema wananchi wanaolipwa fidia hizo wakawa waaminifu ili kufanya zoezi hilo la kuanza miradi kuendelea.

Aidha kwa upande wa Waziri wa Viwanda amesema mradi huo umekuwa ukiandikwa kwenye vitabu na kuwepo kwenye dira ya Taifa ya miaka 25  ambapo tangu mwaka 2000 uliandikwa uanze kutekelezwa.

Amesema mradi huo utakapokamilika utaokoa fedha nyingi za kigeni zaidi ya dola Bl. 1 ambazo zimekuwa zikitumika kwa mwaka mzima katika uagizaji wa bidhaa za chuma hivyo badala ya kuendelea kupoteza fedha hizo zitaelekezwa katika huduma nyingine za kijamii.

"Taifa lipo katika hali ngumu kwa sasa ya upatikanaji wa dola za kimarekani lakini sisi tunatumia dola za kimarekani zaidi ya Bl. 1 kwa mwaka kwa kuagiza chuma ambacho tayari tunacho imefika wakati sasa watumishi wenzangu ndani ya wizara na NDC  tuseme basi inatosha hakuna muda tena wa kusubiri na majadiliano yasiyo na kikomo", alisema Dkt. Kijaji.

Naye mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ameiomba serikali kupitia Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Ashatu Kijaji kutenga maeneo na kuwagawia vitalu wachimbaji wadogo wa wilaya ya Ludewa na mkoa wa Njombe ili nao waweze kunufaika na uchimbaji huo.

" Tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha hili lakini pia napenda niwaambie wananchi kuwa namba 10 mgogoni mliyonipa  nitaendelea kuicheza  vyema, lakini pia Mheshimiwa Waziri kama unavyoona leo hii wafanyabiashara wamejaa hapa kwa wingi, lengo lao ni kusikia ni lini miradi hii itaanza rasmi na namna ambavyo wanaweza kutengewa vitalu kwaajili yao ".

Aidha kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Njombe Deo Mwanyika amesema wabunge wote wa mkoa huo waliungana kusukuma jambo hilo huku mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akipewa jukumu la kuhakikisha suala la ulipwaji fidia linakamilika.

"Sisi wabunge wa mkoa wa Njombe tulikuwa na agenda zetu za kimkoa ikiwemo hii ya Liganga na Mchuchuma ambapo wote kwa pamoja tulilisemea hili lakini mbunge Kamonga ndiye alilibeba zaidi na hatimaye fidia hizi leo zinaenda kulipwa".

Hata hivyo kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) Nicolaus Shombe amesema mwaka 2013 ilifanyika tafiti katika miradi hiyo na kugundua kuwa katika upande wa Mchuchuma kwenye makaa ya mawe kuna Tani Ml. 428 kwenye eneo la km za mraba 30 ambayo yanatarajiwa kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 140 huku chuma cha liganga kikiwa na ukubwa wa zaidi ya Tani Ml. 126 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa miaka isiyopungua 56.

Sanjali na hilo alisema wananchi wanaopisha miradi hiyo tayari wameshaanza kulipwa fedha zao kwa njia ya mfumo ambapo mpaka usiku wa tarehe 6 mwezi huu tayari watu 39 walikwisha ingiziwa malipo kwenye akaunti zao huku wengine wakiendelea kuingiziwa ambapo ndani ya siku tano wananchi wote watakuwa wamekwisha lipwa.

Nao wananchi wameonekana kufurahishwa na hatua hiyo iliyofikiwa huku wakipongeza serikali ya Rais Dkt. Samia sambamba na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga.

Share To:

Post A Comment: