Kufuatia mauaji ya kikatili ya kukatwa mapanga, Dk Isack Sima wa kituo cha afya Nyang’oto kilichopo Kata ya Nyamongo, Tarime Vijijini, Mkoa wa Mara, wizara ya afya imelaani tukio hilo na kuelezea uchunguzi unafanyika.

Dk Sima aliyekuwa Mganga Mfawithi wa kituo hicho, ameuawa kwa kukatwakatwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiojulikana wakati akitoka kituo chake cha kazi usiku akirejea nyumbani Mei 3, 2023.

Leo Jumamosi, Mei 6, 2023 Wizara ya Afya kupitia taarifa iliyotolewa kwa Umma na Kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa sekta hiyo, Aminiel Aligaesha imebainisha imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya mauaji ya kikatili ya mtaalamu huyo wa afya.

"Wizara ya afya inalaani vikali kitendo hiki cha mauaji ya mwanataaluma ya udaktari na kitendo hiki hakikubaliki kwenye jamii," imeeleza taarifa hiyo.

Kupitia taarifa hiyo, Serikali kupitia vyombo vyake inafanya ufuatiliaji dhidi ya mauaji hayo na taarifa rasmi itatolewa.

Baadhi ya watu wanaomfahamu daktari huyo walimuelezea ilikuwa ni kawaida kwake kujitolea kuwasaidia wagonjwa hata kwa muda wa ziada.

Siku ya tukio la mauaji ya mtaalamu huyo wa afya inaelezwa akiwa kwenye usafiri wake wa pilipiki, alikutana na watu waliomsimamisha na kumshambulia kwa mapanga kichwani, mgongoni, mikononi na miguuni.

Imeelezwa Dk Isack baada ya kuhitimu shahada ya udaktari Chuo Kikuu cha Mtakatifu Francisko cha Afya na Sayansi Shirikishi (SFUCHAS) na mafunzo kwa vitendo aliajiriwa kituo cha afya Nyang'oto kata ya Nyamongo, Tarime vijijini ambako amefanya kazi kwa miaka miwili kama Mganga Mfawidhi.

Share To:

Post A Comment: