WIZARA YA ELIMU YAIOMBA BUNGE KUIDHINISHA BAJETI YA TRILIONI 1.6  KWA MWAKA WA FEDHA 2023/2024


Na; Elizabeth Paulo, Dodoma 


Serikali imeendelea kuchochea maendeleo ya sayansi, Teknolojia na Ubunifu Kwa kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu nchini kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeliomba Bunge kuidhinisha jumla ya Shilingi Trilioni 1.67 kwa ajili ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo kwa Mwaka wa fedha wa 2023/24.


Hayo yameelezwa leo Mei 16, 2023 na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo Bungeni Jijini Dodoma kwa mwaka wa fedha 2023/2024.


Prof. Mkenda amesema katika mwaka wa fedha 2023/24, Wizara imepanga kutekeleza vipaumbele vitano vyenye lengo la kuongeza ubora wa Elimu, Kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata Maarifa, Ujuzi, Kujiamini, Kujiajiri, na Kuajirika.


"Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni kukamilisha mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu na kuanza utekelezaji, Kuongeza fursa na ubora wa Mafunzo ya Amali (Ufundi) katika elimu ya Sekondari na Vyuo vya kati vya Amali". Amesema Prof. Mkenda


Amesema Serikali itaendelea kuongeza fursa za elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini kwa kuendelea kusajili na kudahili wanafunzi katika vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.


"Ili kuwezesha utekelezaji wa malengo kwa mwaka wa fedha 2023/24 , Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 1,675,753,327,000.00 kwa mchamganuo ufuatao, Shilingi 537,880,762,000.00 ni kwaajili ya Matumizi ya kawaida ya Wizara ambapo shilingi 500,957,569,000.00 ni kwaajili ya Mishahara huku shilingi 36,923,193,000.00 ni kwaajili ya Matumizi Mengineyo na shilingi 1,137,827,565,000.00 zinaobwa kwaajili ya miradi ya Maendeleo". Amesema Prof. Mkenda 


Prof. Mkenda amesema katika katika kusimamia na kuendeleza elimu ya ualimu nchini, Serikali imewezesha huduma ya chakula kwa wanafunzi 22,085 katika vyuo vya Ualimu vya Serikali 35 pamoja na Mafunzo kwa vitendo ( Block Teaching Practice -BTP) kwa wanafunzi 17,631 wa vyuo vya Ualimu 35 vya Serikali.


Aidha Prof. Mkenda amesema Serikali imeendelea kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa katika ngazi ya Awali ,Msingi, na Sekondari inaendana na mahitaji ya sasa na kufikia azma hiyo Serikali imekamilisha uandikishaji wa mihtasari 70 katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari Kidato Cha 1-6.


Prof.Mkenda amesema kuwa ,Serikali itaanza kusajili shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa mfumo wa kielektroniki kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuwafikia wadau wengi zaidi. Pia, itanunua magari 12 na kuweka samani katika ofisi 195 za uthibiti ubora wa shule kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji wa kazi.




Aidha ,Serikali itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka 202,877 hadi 210,169, itaendelea kusajili wanafunzi 72,361 wa mwaka wa kwanza katika mfumo wa malipo wa kidijitali (DIDiS) na itaboresha mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Mikopo na utunzaji wa nyaraka (iLMS, MUSE, DIDis) Gateway, OLAMS, MEL na eDMS kuwa wenye ufanisi na tija.



Serikali itaendelea kutoa fursa za Elimu ya Juu kwa wanafunzi wenye ufaulu uliojipambanua kutoka wanafunzi 593 hadi 1200 kupitia Samia Skolashipu na itajenga kampasi 14 za vyuo vikuu katika mikoa ambayo haina kwa lengo la kuleta mageuzi ya kiuchumi.

Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: