Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza utalii wa ndani ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora zenye gharama nafuu kwenye vivutio hasa huduma za malazi, chakula, usafiri na viingilio.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Chillo (Mb) kwa Niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, Ameir Abdallah Ameir aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha utalii wa ndani unaimarika.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuhamasisha makundi mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na wanafunzi, wajasiriamali, wafanyakazi na makundi maalum kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii na kufanya mikutano.

Pia, amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma na kutumia chaneli maalum ya kutangaza utalii (Tanzania Safari Channel) kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii pamoja na kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio hivyo.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuongeza maeneo ya utalii, kuibua vivutio na mazao mapya ya utalii na kuendeleza miundombinu ya utalii katika kanda zote za utalii nchini.

Kuhusu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini, Mhe. Prof. Patrick Ndakidemi, aliyeulizia mpango wa Serikali wa kutatua kero ya nyani, kima, tumbili na ngedere kwa Wananchi wanaopakana na Mlima Kilimanjaro, Mhe. Chillo amesema kuwa Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro ina vituo vya askari wanyamapori kwenye Wilaya zote zinazopakana na hifadhi ambavyo kwa kushirikiana na maafisa wa wanyamapori kutoka Wilaya husika askari wanyamapori wamekuwa wakifanya kazi ya kuwafukuza wanyamapori wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi ya Wananchi au mashamba yao.

Mhe. Chillo ametoa wito kwa Wananchi wa Jimbo la Moshi Vijijini wanaopatwa na madhara ya wanyamapori wakiwemo nyani, kima, tumbili na ngedere kutoa taarifa kwa Askari wa Uhifadhi wa vituo hivyo pale wanyamapori hao wanapoingia kwenye maeneo yao ili waweze kudhibitiwa

Share To:

Post A Comment: