Happy Lazaro,Arusha.

Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi Vijana Ajira na wenye ulemavu,Prof Joyce Ndalichako,amevitaka vyuo  vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini kuimarisha elimu ya ujuzi kwa wanafunzi ili kuzalisha wataalam wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali na kukidhi mahitaji ya soko la ajira.

Pro Ndalichako ameyasema hayo leo  Mei 16,2023 jijini Arusha,akifungua kongamano la elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).

Amesema ni muhimu wadau kuangalia namna ya kushirikiana kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili yawe na ujuzi unaohitajika huku akisisitiza malengo ya serikali katika sekta ya elimu ni pamoja ya kuhakikisha elimu inatoa ujuzi na nguvukazi inayohitajika katika soko la ajira.

"Mmekuwa mkishuhudia malalamiko kutoka kwa waajiri wakisema kwamba wahitimu hawana ujuzi unaotakiwa,hii ni zaidi ikiwemo kwenye sekta ya kilimo,uchukuzi,utalii,usafirishaji,muweke mikakati ya kuangalia namna ya kuimarisha ujuzi kwa vijana ambao unatakiwa katika soko la ajira ili watumie ujuzi huo katika kuleta tija na maendeleo,"amesema

Awali Katibu Mtendaji wa NACTVET,Dk Adolf Rutayuga,amesema kongamano hilo limeshirikisha wadau zaidi ya 300, kutoka ndani na nje ya nchi ambao watajadiliana mada mbalimbali zinazohusu ujenzi wa ujuzi na umahiri kwa vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi stadi.

 Kaimu Mkurugenzi wa ufuatiliaji wa rasilimali na miradi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA),Masoni Nyirenda,amesema wanasimamia mfuko wa kuongeza ujuzi ambao unafadhili taasisi mbalimbali za mafunzo kwa ajili ya kusaidia vijana waweze kupata mafunzo na kujenga uwezo wa taasisi kuweza kutoa elimu yenye ubora ya ujuzi.

"Tunajua mausala ya ajira nchini yamekuwa changamoto  na suala la ujuzi lilionekana ni changamoto kubwa sana  kwa hiyo kupitia mfuko ule tumefadhili vijana zaidi ya 48,000 nchi nzima kupata mafunzo ya ujuzi,"amesema

Share To:

Post A Comment: