Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewasilisha hoja ya makadirio ya bajeti ya mapato na matumizi ya wizara ya Afya  kwa mwaka 2023/2024 ya Shilingi Trilioni 1.2 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma.

”Mheshimiwa Spika, jumla ya fedha zote zinazoombwa na Wizara ni Shilingi 1,235,316,516,000 ili kuweza kutekeleza malengo iliyojiwekea” amesema Waziri Ummy Mwalimu akiwa anawasilisha hoja yake bungeni.

Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa rasilimali na kuboresha zaidi Sekta ya Afya nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya Wizara ya Afya ambayo imeongezeka kutoka Shilingi Trilioni 1.1 mwaka 2022/23 hadi Shilingi Trilioni1.2 mwaka 2023/24.

Amebainisha kuwa kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 732 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya Sekta ya Afya nchini huku Shilingi Bilioni 502 zikiwa zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Kuhusu ukusanyaji wa maduhuli, Waziri Ummy amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24 Wizara na Taasisi zilizo chini yake imekadiria kukusanya kiasi cha Shilingi Bilioni 677 kutoka kwenye vyanzo vyake.

”Vipaumbele vya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2023/24 tutajikita kuimarisha huduma za Kinga dhidi ya magonjwa ikiwemo huduma za chanjo, huduma za lishe, huduma za usafi na afya mazingira na huduma za afya ngazi ya jamii” amesema Waziri Ummy.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya umma katika ngazi zote,Kuimarisha upatikanaji na udhibiti wa dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na damu salama katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya; Kuimarisha huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga; Kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi ili kusogeza huduma hizi karibu na wananchi na kuwapunguzia gharama za kupata matibabu haya nje ya nchi; Kuimarisha huduma za Afya ya Akili, huduma za utengamao na Tiba Shufaa.

Ameendelea kusema kuwa Wizara itaendelea kudhibiti magonjwa ya mlipuko na magonjwa hatari ya kuambukiza; Kudhibiti magonjwa ya kuambukiza hususani Malaria, Kifua Kikuu (TB), VVU/UKIMWI na Homa ya ini; Kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususani kisukari, shinikizo la juu la damu na magonjwa ya Moyo na kuimarisha huduma za dharura nchini ikiwemo ajali; Kuimarisha upatikaji wa wataalam katika Sekta ya Afya katika fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi.

”Wizara itaendelea na kusimamia huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini; Kuimarisha Mifumo ya TEHAMA na matumizi ya takwimu; Kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini; Kusimamia tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za Afya” amefafanua Waziri Ummy.

Share To:

Post A Comment: