Na Denis Chambi,Tanga.

Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete  ameliagiza shirika la Reli Tanzania mkoa wa Tanga kuhakikisha ikarabati kipande cha reli kinachotoka kituo kikubwa cha Mkwakwani hadi  bandari ya Tanga hii ikilenga hasa  kuongeza kasi ya usafirishaji wa mizigo inayotoka na kuingia katika bandari hiyo.

Alitoa maagizo hayo  april 1,2023 mara baada ya kutembelea   mradi wa ukarabati katika bandari hiyo  ambapo kwa sasa umefikia  asilimia 98.9  katika utekelezaji wake ikiwa ni uboreshaji wa gati  2 kutoka urefu wa kilomita   1.7 hadi kilomita 450 pamoja na kuongeza kina cha bandari kutoka mita 3 hadi 13 mradi wote ukigharimu jumla ya shilingi Billion 429.1 zilizotolewa na serikali.

Mamlaka ya Bandari ambayo ilikiri kupokea mapendekezo hayo ya ukarabati wa kipande hicho cha reli hivi karibuni kutoka shiria la reli ilieleza mbele ya naibu waziri kuwa itakaa na ndani ya wiki moja na kutoa  majibu ya  ukarabati huo huku Naibu waziri akizipunguza siku hizo na kuwaagiza ndani ya siku tatu kuja na majibu kamili ya nini kifanyike ili kuweza kukamilisha mradi huo. 

Hata hivyo shirika la reli ambalo limeshapeleka mapendekezo ya gharama kwaajili ukarabati wa kipande cha reli hiyo kinachotoka kituo kikubwa hadi bandarini hapo   tayari  TPA wameshatenga kiasi cha shilingi Million 500 kwaajili ya kazi hiyo.

"Nimewapa maelekezo watu wa Reli kwamba walichelewa kuleta mapendekezo kwa mamlaka ya Bandari na Mamlaka ya Bandari wana fedha kwaajili ya zoezi hilo na wamesema ndani ya wiki moja watakuwa  wameshazipitia ili  watu wa reli waanze kufanya hiyo kazi na mimi nimesema sio wiki moja,  wiki moja ni mbali fanyeni ndani ya siku tatu muwe mmeshawarudishia majibu watu wa reli ili waanze  kuihuisha reli iliyokuwepo zamani ndani ya bandari hii ya Tanga" alisema Mwakibete.

Uboreshaji wa bandari hiyo umeanza kuzaa matunda kwani kwa kipindi cha mwezi january hadi march 2023  wamefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi billion 5 ikivunja rekodi zaidi ya kupokea meli kubwa  ambapo hivi karibuni ilipokea Meli Metsovo  iliyotokea nchini Marekani yenye ukubwa wa Mita 189.9 ikiwa imebeba malighafi zinazotumika viwandani pamoja na meli nyingine mbili ambapo awali hazikuweza kufika kutokana na kina kidogo cha Bandari hiyo.

Awali akizungumza Mhandisi kutoka shirika la Reli "TRC' Patience Karumuna
alisema kuwa mara baada ya kupokea maagizo kutoka kwa Makamu wa Rais Philipo Mpango mwishoni mwa Mwaka jana walifanya  usanifu wa kujua mahitaji  ya kipande hicho kinachoenda bandarini ambapo walifanikiwa kukamilisha na kuikabidhi mamlaka ya Bandari ya Tanga.

" Baada ha kupokea maagizo kutoka kwa makamu wa Rais ilikuwa mwezi December upande wa shirika tukishirikiana na  TPA hatua za  kwanza kabisa tulizofanya ni kurudishia miundombinu ya reli upande wa stesheni na tumekamilisha ,   kwa upande wa  Bandari tumeleta wasanifu wakaja  tukaangalia mahitaji yaliyopo kwa sasa hivi   tukatengeneza makisio ya gharama ambalo nalo tumelikamilisha tumeikabidhi  mamlaka ya Bandari 'TPA' kwaajili ya wao  waweze kulipitia "alisema Karumuna

Akizungumza kaimu Meneja wa bandari ya Tanga Petter Milanzi aliishukuru serikali kwa uwekezaji na maboresho makubwa hayo yaliyofanyikia ambayo sasa matunda yake yanaonekana huku akiwakaribisha wadau na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuitumia bandari hiyo.

"Sisi kama  Bandari tunatoa wito kwa wadau wetu wote na watumiaji wa bandari kwamba bandari ya Tanga imeshafunguka tupo tayari kuwahudumia na kutoa huduma bora ,  tumeshajiandaa kukabiliana na ushindani ili kuweza kuwahudumia wateja wetu vizuri,  tunajua serikali imewekeza fedha nyingi kwahiyo fedha zile zilizowekezwa lazima zitoe faida hivyo sisi kama bandari ya Tanga lazima tutoe uhakika kuwa tupo tayari kufanya kazi ili bandari hii iwe inaleta faida kubwa kadiri ya kilichowekezwa" alissma Milanzi.
 
 
 
 
 Kaimu meneja wa bandari  Tanga Petter Milanzi akitoa maelezo kwa Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete wakati alipofanya ziara ya yake ya  siku moja kutembelea mradi unaoendelea katika bandari hiyo april 1,2023.
 
 
 Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete akipata maelezo kutoka kwa mhandishi wa shirika la Reli Patience Karumuna kuhusu miundombinu ya reli ambayo inatakiwa kufika bandarini hapo ili kuzidi kurahisisha usafirishaji.
 
 
 Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi Atupele Mwakibete akipata maelezo kutoka kwa meneja wa mradi wa Rafael Angulo Niras Resident wanaotekeleza mradi katika bandari ya Tanga ambao mpaka sasa wamefikisha asilimia 98.9.
Share To:

Post A Comment: