Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick akitoa chanjo kwa mmoja wa watoto kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya chanjo duniani yaliyofanyika kimkoa Kata ya Iyumbu wilayani Ikungi mkoani hapa Aprili 24, 2023.

................................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKOA wa Singida unatarajia kuwachanja watoto wote 36,350 walio chini ya miaka mitano ambao hawakupata chanjo na watoto ambao wanaendelea na ratiba za chanjo zao pamoja na chanjo ya UVIKO-19.

Hayo yamesemwa Aprili 24, 2023 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye alikuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya chanjo duniani yaliyofanyika kimkoa Kata ya Iyumbu wilayani Ikungi mkoani hapa.

Dk. Ludovick alisema maadhimisho hayo yanawalenga watanzania wote kutambua umuhimu wa chanjo katika kukinga milipuko ya magonjwa na hivyo kuzuia ulemavu na vifo vinavyozuilika hasa kwa makundi maalum kama watoto wenye umri chini ya miaka mitano, watoto wa kike wenye umri chini ya miaka 14 na kwa chanjo ya UVIKO 19 watu wazima kuanzia miaka 18 lakini hasa kwa watoto wadogo zaidi na makundi yaliyotajwa hapo.

"Takwimu za utafiti wa magonjwa mengi ya kuambukizwa yanayozuilika kwa chanjo huathiri zaidi watoto wadogo hasa wenye umri chini ya miaka mitano, hivyo basi chanjo huwapatia kinga ya ziada dhidi ya magonjwa hayo," alisema Ludovick.

Alisema pamoja na muitikio mkubwa wa wananchi kwenye kampeni mbalimbali za chanjo, takwimu zinaonesha uwepo wa mlipuko ya ugonjwa wa surua na Rubella katika Halmashauri za Wilaya za Ikungi, Itigi na Singida DC hivyo kuonesha bado kuna haja kubwa ya kutoa elimu na kampeni za mara kwa mara kwenye jamii juu ya umuhimu wa watoto kukamilisha chanjo mbalimbali.

Dk.Ludovick alisema katika halmashauri hizo watu takribani 150 walibainika kuwa na dalili za ugonjwa wa Surua Rubella na eneo la Kata ya Iyumbu kupitia vijiji vya Msake na Iyumbu vilionekana kuwa na watoto wengi ambao hawakupata dhidi ya Surua Rubella.

Aidha Dk.Ludovick alitumia nafasi hiyo kuipongeza Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kuratibu maadhimisho hayo kitaifa.

Pia alitoa pongezi kwa kamati ya maandalizi ya Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa maandalizi mazuri kwa kushirikiana na Mdau wa Afya ndani ya Mkoa JHPIEGO kwa jitihada zao zilizofanikisha uzinduzi wa maadhimisho hayo.

Dk. Ludovick alisema watalaam wa afya Mkoa wa Singida wamejipanga vizuri, sio tu kutoa chanjo bali hata kutoa huduma nyingine za afya zikiwemo kutoa elimu ya afya kuhusu umuhimu wa kumaliza chanjo kwa watoto na madhara ya watoto kutokumaliza chanjo, uchangiaji wa damu salama, afya ya uzazi, lishe, magonjwa sugu yasiyoambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu,malaria na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Singida, Habibu Mwinorya alisema malengo ya maadhimisho hayo ni kuwafikia watoto wote chini ya miaka mitano na watu wenye umri wa miaka 18 na kuendelea katika chanjo za UVIKO 19 kwa kuwachanja watoto wote 36,350 walio chini ya miaka mitano ambao hawakupata chanjo tangu  mwaka 2019.

Alisema malengo mengine ni kuwachanja watoto wote 6,535 waliokosa chanjo chini ya miaka mitano tangu mwaka 2019 hadi sasa na kuwapatia chanjo watoto wote waliopo katika ratiba zao za kliniki za kila mwezi hasa za mwezi Aprili, 2023.

Aidha, Mwinorya alisema lengo lingine ni kuhakikisha watoto wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ambao hawajapata ama kukamilisha chanjo dhidi ya UVIKO-19 wanachanja na watoto wote ambao walichanja kipindi cha zoezi la pili lililofanyika Machi 24 na 30, mwaka huu wanarudia kukamilisha kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayozuilika kwa chanjo.

Alisema kufikia mwaka 2023 Machi Mkoa wa Singida umeongeza idadi ya vituo vinavyotoa huduma za chanjo kutoka vituo 218 mwaka 2021 hadi vituo 237 sawa na asilimia 89 ya vituo 266 vinavyotoa huduma za afya na hiyo ni kutokana na vituo vilivyojengwa katika Awamu ya Sita chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ambapo kuna vituo vipatavyo 29 vinavyotoa huduma lakini havina majokofu ya chanjo.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Samson Michael akitoa chanjo.
Muuguzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Iyumbu, Kundi Kazimili, akitoa chanjo. Aliye mpakata mtoto anayepewa chanjo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick  akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Singida, Habibu Mwinorya, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Afisa Tarafa ya Sepuka, Cornel Nyoni ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ikungi katika uzinduzi huo akizungumza.
Wanafunzi wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi huo ukiendelea.
Wananchi wa Kata ya Iyumbu na maeneo ya jirani na kata hiyo wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Maombi ya kuombea uzinduzi huo yakifanyika.
Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Kata ya Iyumbu na vijiji jirani wakiwa kwenye uzinduzi huo wa chanjo.


Wataalam wa Kata ya Iyumbu wakitambulishwa kwenye uzinduzi huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga.akizungumzia umuhimu wa wananchi kujitokeza kupata chanjo hiyo.
Chanjo ikiwa imebebwa baada ya kuzinduliwa.
Wakina mama wakiwa wamewabeba watoto wao wakisubiri kupatiwa chanjo hiyo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika uzinduzi huo, Dk.Anthony Mwangolombe (kushoto) na Diwani wa Kata ya Iyumbu, Peter Kwiligwa wakiwa wamewapakata watoto wakatiwakisubiri kupatiwa chanjo.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga (kushoto) akiwa na Diwani wa Kata ya Mwaru, Iddi Makangale wakiwa kwenye uzinduzi wa wiki ya chanzo hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Iyumbu, Ayub Seleman akitoa chanjo kwa mmoja wa watoto wakati wa uzinduzi wa utoaji wa chanjo hiyo.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick akikabidhiwa zawadi ya mbuzi na viongozi wa Kata ya Iyumbu.
 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: