Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameielekeza Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) kujenga nyumba za watumishi kwenye maeneo yenye fursa na mazingira mazuri ya kuishi ili kuwawezesha watumishi wote hata walio kwenye maeneo ya pembezoni kupata makazi bora ya kuishi yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu.


Mhe. Kikwete ametoa maelekezo hayo leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kujitambulisha na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa Watumishi Housing Investments jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kikwete amesema pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na inayoendelea kufanywa na Watumishi Housing Investments, ni vizuri zaidi wakafikiria kujenga nyumba nyingi zaidi maeneo yenye uhitaji
mkubwa wa nyumba hizo, akitolea mfano wa maeneo ya pembezoni mwa nchi ambayo ndio yenye uhitaji mkubwa wa nyumba.

“Mnafanya kazi nzuri sana ya ujenzi wa nyumba hizi, lakini mnatakiwa kuangalia fursa, maeneo gani yana uhitaji mkubwa wa nyumba, hasa maeneo ya pembezoni ili hata wanaohamishiwa huko wafurahie maisha na kutekeleza kikamilifu jukumu la kutoa huduma bora kwa wananchi,”
Mhe. Kikwete amesisitiza.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa, pamoja na haki na stahiki nyingine wanazopata watumishi, mazingira mazuri ya kuishi ni jambo lingine la msingi ambalo linapaswa kupewa kipaumbele na WHI wakati wa
utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa nyumba za kuishi watumishi wa umma.

Mhe. Kikwete amesema ni matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona watumishi wa umma wanafanya kazi kwa bidii na maarifa, hivyo katika kufikia malengo ya Mhe. Rais, Watumishi Housing Investments wana nafasi kubwa ya kuunga mkono lengo hilo la Mheshimiwa Rais kwa kujenga nyumba bora kwa ajili ya kuziuza na kuwapangisha watumishi wa umma nchini.

“Taasisi zinazojenga nyumba ziko nyingi, wengine wanajikita kwenye ujenzi wa nyumba kwa ajili ya mwananchi yeyote lakini sisi Watumishi Housing Investments tuna malengo yetu ambayo yamejikita kwa
watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, hivyo tunapaswa kuhakikisha malengo ya taasisi yanatimia.

Mhe. Kikwete ameisisitiza Menejimenti ya taasisi hiyo kutosita kuwashirikisha Viongozi na Menejimenti ya Ofisi ya Rais, menejimenti yaUtumishi wa Umma na Utawala Bora pale wanapokutana na changamoto au kama kuna mwongozo wowote wanaouhitaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, Mhe. Kikwete ameitaka taasisi hiyo kutangaza utekelezaji wa majukumu ya taasisi yao ili yafahamike kwa wahusika.

“Watumishi wanahitaji kuyajua majukumu yenu, mjitahidi kujitangaza ili kuwafikia kiurahisi tunaowalenga na kuifanya taasisi yetu kuwa kimbilio la watumishi pale wanapohitaji kuwa na nyumba iwe ya kununua au kupangisha,” Mhe. Kikwete amefafanua.

Mhe. Kikwete amehitimisha ziara yake ya kikazi ya kuhimizia uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi za umma zilizo chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora jijini Dar es Salaam.
Share To:

Post A Comment: