Vurugu zimezuka katika Kijiji cha Engikaret Wilayani Longido Mkoani Arusha baada ya wananchi 10 kukamatwa kwa madai kuwa walikuwa wakizuia wataalamu wa mradi wa umeme wa KV400 unaotoka Mkoani Singida hadi Mji wa Namanga kufanya kazi kwa madai kuwa mradi huo umepita katika maeneo yao ambayo hadi sasa hawajalipwa fidia ya shilingi bilioni 1.8 zilizotolewa na serikali.

Akizungumza kwa simu ya kiganjani na mwandishi wetu ,Thomas Mollel alisema kuwa wananchi hao kweli walifanya hivyo kwa kuwa eneo linalopita mradi ni mali yao na sio mali ya kijiji kama inavyotangazwa na baadhi ya viongozi wa serikali kijiji,Kata na Wilaya.

Alisema fedha Bilioni 1.8 zilizotumwa na Wizara ya Nishati kwa mwananchi wa Kijiji cha Engikaret kwa ajili ya fidia ya ardhi kupisha mradi huo zilifuata taratibu zote za tathimini ikiwa ni pamoja na kupigwa picha wananchi 46 na tathimini hiyo ilifanywa na maofisa wa idara ya Ardhi Longido na ndio maana serikali ilituma fedha hizo kwa wananchi hao.

Mollel alisema polisi wakiwa katika gari walikwenda na kuwazomba watu 10 waliokuwa wakiwazuia wataalamu hao kuendelea na mradi huo na kusema kuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido bado hajajua kiini cha mgogoro huo kwani kwa asilimia kubwa anapotoshwa.

Alisema aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati katika serikali ya awamu ya tano ,Dkt Medadi Kalemani alikwenda kijiji hapo katika Mkutano wa hadhara na kusema kuwa fedha za fidia bilioni 1.8 ni za wananchi wa Kijiji hicho na kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo kipindi hicho ,Frank Mwaisumbe kuhakikisha anasimamia hilo ili wananchi hao walipwe stahiki zao.

Mwananchi huyo alisema na kushangazwa kuona fedha hizo zilipokelewa Longido lakini wananchi hao hawakupewa haki yao hadi jana na maeneo yao kutumika kupisha mradi yakichukuliwa kibabe bila ya kulipwa fidia kama serikali kuu ilivyoagiza.

‘’Pesa ilitolewa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais marehemu Dk John Magufuli lakini watendaji wa wilaya ya Longido wanajua walizitumiaje hizo pesa ila tunamwomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuliangalia hilo na wananchi wenzetu kupata stahiki zao’’ alisema Mollel

Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu ya kiganjani ,Mkuu wa Wilaya ya Longido ,Marco Ng’umbi Mkalimoto alisema kuwa hakuna mtu hata mmoja aliyekamatwa na polisi katika mradi huo bali yeye alikuwa hapo na kikao na wataalamu wa mradi huo , viongozi wa serikali ya Kitongoji,Kijiji na Kata Engikaret na alitoa maagizo kwa viongozi hao kuhakikisha mradi huo unaendelea bila ya vikwazo vyovyote.

Mkalimoto alisema kuwa uamuzi huo ni baada ya serikali kupata taarifa kuwa kuna mtu analeta vurugu katika Kijiji cha Engikaret na kuwazuia wataalamu kushindwa kutekeleza mradi huo kwa madai kuwa eneo linalopita mradi ni mali yake wakati sio kweli kwani eneo hilo ni mali ya serikali ya Kijiji cha Engikaret.

‘’Hakuna watu waliokamatwa ila kuna mtu ndio alikuwa akikwamisha wataalamu kuendelea na maradi na nimekwenda sikumkuta na nimeagiza viongozi wa Kitongoji,Kijiji na Kata kusimamia mradi na atakayeleta vurugu za kuwazuia wataalamu akamatwe ‘’alisema Mkalimoto

Share To:

Post A Comment: