Baadhi ya wanafunzi wa darasa la Awali wakiendelea kujifunza ikiwa ni hatua yao ya awali katika elimu ya msingi. 

Na Abby Nkungu, Singida
 

KUANZISHWA kwa shule shikizi tisa katika Manispaa ya Singida kumetajwa kuwa ni mwarobaini kwa watoto walio chini ya miaka minane kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku kufuata elimu kwenye shule mama, kuimarisha ulinzi na usalama wao na kupunguza utoro na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Afisa elimu Msingi katika Manispaa ya Singida, Omary Maje alibainisha hayo wakati akizungumzia mafanikio na changamoto za shule shikizi katika halmashauri hiyo.

“Kuanzia mwaka 2017 hadi sasa, tumefanikiwa kuwa na shule shikizi tisa ambazo kwa kweli zimesaidia watoto wadogo; hasa wa chekechea, wa darasa la kwanza na la  pili kutembea umbali mrefu kutafuta elimu; hivyo kumaliza utoro, vitendo vya ukatili wa kijinsia njiani au usalama wao kuwa mashakani wanapokutana na wanyama kama fisi” alisema.

Alieleza kuwa baadhi ya shule za msingi mama zipo umbali wa kilomita 5; hivyo ilikuwa  vigumu kwa watoto  wenye umri wa chini ya miaka minane kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 kila siku kufuata elimu; hivyo Manispaa kuamua kuanzisha shule shikizi jirani na makazi ya watu kuondoa changamoto hiyo.

Maje alizitaja shule hizo Shikizi kuwa ni pamoja na Mnung’una, Mughenyi, Manguampyughu, Sundu, Mwembemoja, Mwachichi, Nkuhi, Mwaghumpi na Makyunje ambazo hadi hivi sasa zina jumla ya wanafunzi 2,665 kati yao wavulana ni 1,316 na wasichana 1,349.

Alisema kuwa kuendelezwa kwa shule hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya mwaka 2021, ambayo pamoja na mambo mengine, inaweka mkazo zaidi kwenye kuimarisha ulinzi na usalama, afya, lishe bora, elimu na malezi yenye mwitikio kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 8.

Hata hivyo; anakiri kuwa bado shule hizo shikizi zinakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo   kutokuwa na miundombinu ya kutosha kama madarasa, vyoo na nyumba za walimu huku zikiwa hazina fungu la uendeshaji hivyo kuendelea kutegemea fungu lililoko shule mama na hakuna walimu wa kudumu kwani walimu wake hutegemea zaidi kutoka shule mama na wale wa kujitolea.

Baadhi ya wazazi na walezi wanaipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha shule  shikizi ili kupunguza changamoto kwa watoto na kuomba ziboreshwe na kusajiliwa kuwa shule kamili.

“Mimi mtoto wangu aliponea pale Mwembemoja ndio ikawa nafuu; vinginevyo ilikuwa aache shule kabisa au nimtafutie hizi za kuchukuliwa na magari maana mtoto alikuwa akitembea zaidi ya kilomita saba kwenda tu bado kurudi, akija nyumbani amechoka mpaka basi” alisema Halima Ali mkazi wa Mtipa Singida na kuongeza kuwa sasa shule hiyo imepata usajili kamili.

Naye, Ibrahimu Loth mkazi wa Mwenge anapongeza kuanzishwa kwa shule hizo shikizi kwani kwa dunia ya sasa watoto wadogo kutembea umbali mrefu  ni hatari  kwani wanaweza kufanyiwa vitendo  vya ukatili ikiwemo ulawiti, kubakwa au kujeruhiwa na wanyama.

Walimu wa shule  za  awali na msingi katika Manispaa ya Singida wanasema kuwa  shule shikizi zinaweza kusaidia kuinua kiwango cha elimu kwani awali watoto walikuwa wanafika shule wakiwa wamechoka kwa kutembea umbali mrefu na muda wote wakipiga miayo tu darasani kwa uchovu na njaa.

“Mengine huwa hatusemi tu ingawa tunaumia maana na sisi pia ni wazazi. Ukipewa kufundisha darasa la awali na la kwanza duh! ikifika saa 4 asubuhi watoto wote wanaotoka mbali  unakuta wanachapa usingizi darasani na walio macho ni miayo kwa kwenda mbele, ila sasa kwa hizi shikizi watoto hawatembei umbali mrefu hivyo hawachoki, tunaishukuru Serikali” alisema mmoja wa walimu hao.

Kulingana na taarifa za  idara ya elimu Manispaa ya Singida, kati ya shule 9 shikizi zilizoanzishwa,  shule 5 tayari zimesajiliwa na Wizara ya elimu kuwa shule kamili huku nyingine zikiwa kwenye mchakato wa kusajiliwa. 


Afisa elimu Msingi katika Manispaa ya Singida, Omary Maje akiwa kwenye moja ya vikao vyake kuelezea umuhimu wa Shule Shikizi

Moja ya shule Shikizi katika Manispaa ya Singida.
 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: