Baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari ya Songo Songo, wawakilishi kutoka PURA na baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya makabidhiano ya vitabu kufanyika.


Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Songo Songo akipokea kitabu kutoka kwa mwakilishi kutoka wa PURA, Mjiolojia Wangese Matiko (aliyevaa miwani). Wengine pichani ni Mku wa Shule ya Songo Songo Sekondari Bw. Said Halfani Rajab (wa kwanza kushoto), wawakilishi wa PURA na baadhi ya walimu wa shule hiyo.

************************

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imechangia vitabu 150 vya sayansi katika Shule ya Sekondari Songo Songo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi. Hatua hii ni kufuatia ombi lililotolewa na uongozi wa shule hiyo wakati PURA ilipofanya ziara ya kikazi shuleni hapo mwaka jana.

Tukio la kukabidhi vitabu hivyo lilifanyika jana, tarehe 09 Machi 2023 katika Shule ya Songo Songo na kuhudhuriwa na baadhi ya walimu wa shule hiyo (akiwemo Mkuu wa Shule Bw. Said Halfan Rajab), wawakilishi kutoka PURA na wawakilishi wa wanafunzi wa shule hiyo.

Akikabidi vitabu hivyo, mwakilishi kutoka PURA, Mjiolojia Wangese Matiko alisema kuwa, PURA inafurahi kuwa sehemu ya wadau walioigusa na kuweka alama katika shule ya Sekondari ya Songo Songo na kwamba PURA itaendelea kushirikiana na shule hiyo kuhakikisha vijana wa Songo Songo wanawezeshwa kielimu.

"PURA kama Mamlaka inatambua mchango wa elimu katika kuandaa vijana kuwa na ujuzi stahiki kwa maendeleo ya sekta zote ikiwemo sekta ya mafuta na gesi asilia na nchi kwa ujumla. Tunaamini kwamba miongoni mwa nyenzo muhimu katika kuwaandaa vijana hawa ni pamoja na uwepo wa vitabu vya kutosha. Hii ndio sababu PURA iliamua kuanza na eneo la kuchangia vitabu." Alieleza Bw. Matiko.

Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Shule, Mkuu wa Shule ya Sekondari Songo Songo Bw. Said Halfan Rajab alisema kuwa mchango wa PURA umewagusa na utasaidia kwa namna moja ama nyingine ongezeko la ufaulu wa wanafunzi, husasan katika masomo ya sayansi kwani shule hiyo ilikuwa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vitabu.

"Kwa niaba ya Uongozi wa shule nitumie fursa hii kuishukuru PURA kwa mchango huu. Tunaipongeza PURA kwa kusimama na ajenda ya elimu kwani yote yanaanza na elimu bora. Uwepo wa wataalamu katika nyanja mbalimbali unategemea sana uwekezaji katika elimu" aliongeza Bw. Said.

PURA kama Mamlaka, pamoja na majukumu mengine, inadhibiti shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Songo Songo ambapo gesi asilia inazalishwa.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: