Na; Elizabeth Paulo, Dodoma


Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekanusha na kutolea Ufafanuzi  taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii hususan Twitter na Instagram kuhusu malalamiko dhidi ya Shirika hilo.


Malalamiko yanayoendelea Kusambazwa katika mitandao hiyo ya kijamii ni pamoja na Mikataba ya mafunzo kazi kwa vijana zaidi ya 400 waliokuwa TASAC ambapo ilivunjwa bila kufuata utaratibu na ikiwa imebaki muda wa mwaka mmoja kuisha kwa mikataba hiyo.


Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Kaimu Abdi Mkeyenge Ameeleza hayo leo Machi 10/2023 Jijini Dodoma,  wakati akitoa ufafanuzi kwa Umma kuhusu Vijana waliokuwa wanafanya shughuli za Mafunzo kazi kwa vitendo ndani ya shirika Hilo.


“Kuna tuhuma zingine walizotoa Vijana hao kuwa walifanya kazi  bila bima ya afya na kwamba TASAC ilitoa rushwa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika mashauri ya kazi yaliyofunguliwa na vijana hao ili haki isitendeke sasa naweza kusema kuwa Hakuna sheria inayomtaka muajiri yeyote yule kumkatia bima ya afya kijana anayefanya shughuli za Mafunzo kazini suala hilo halipo na hakuna taasisi yeyote inayoweza kufanya hivyo kwani stahiki zao zimeainishwa kwenye Muongozo wa Kitaifa wa Mafunzo Kazi uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu na tuhuma kuhusu TASAC kutoa rushwa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ili mashauri ya kazi yaliyofunguliwa na vijana hao haki isitendeke hakuna ukweli wowote”.Alisema Mkeyenge


Mnamo mwezi Julai, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania sura namba 415 kupitia sheria ya fedha namba 5 ya mwaka 2022 kwa kufuta baadhi ya majukumu ya kipekee ya uwakala wa meli, uhakiki wa  shehena /mizigo, udhibiti wa nyaraka na kupunguza wigo wa jukumu la kufanya uwakala wa forodha katika bidhaa zilizokuwa zinagombolewa na kuondoshwa na TASAC chini ya kifungu cha 7 (1) a,b,c na d.


“TASAC kwa kutekeleza mabadiliko ya sheria haya kwakua ilikua inatekeleza majukumu hayo kupitia vijana waliokua wameajiriwa moja kwa moja pamoja na waliokuwa wakifanya mafunzo  kazi lakini kufuatia mabadiliko hayo,  Agosti 11, 2022 TASAC ilivunja mikataba ya mafunzo ya kazi kwa jumla ya vijana 209 waliokuwa wakifanya kazi za uhakiki wa shehena na si zaidi ya 400 kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii”. Alifafanua Bw. Mkeyenge


Mkurugenzi huyo amesema Vijana hao waliandikiwa barua kuwa mikataba yao haitahuishwa tena ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022 kutokana na merekebisho ya Sheria ambayo yamesababisha baadhi ya majukumu ya TASAC kufutwa na kuhamia sekta binafsi.
Bw. Mkeyenge ameongeza kuwa  kati ya vijana 209 waliofutiwa mikataba yao, ni vijana 41  ambao hawakuridhika na maamuzi hayo ambapo Vijana 32 kati ya vijana 41, shauri lao lilifutwa na CMA kwa kuwa liliwasilishwa nje ya muda, hivyo ni vijana 9 ambao shauri lao dhidi ya TASAC lilipokelewa na lipo katika Tume ya Usuluhisi na Uamuzi.


Aidha amesema Vijana 168 waliobaki hawakupinga uamuzi wa TASAC wa kuvunja mikataba yao kutokana na mabadiliko ya Sheria ambayo yalikuwa ni nje ya uwezo wa Shirika.


“Kwa kuwa suala hili lipo kwenye chombo cha maamuzi kisheria, TASAC haipaswi kulizungumzia shauri hilo lakini ilionekana ni busara kulitolea ufafanuzi wa kilichofanyika kwa upande wa TASAC na kuacha hatua za maamuzi zinazoendelea kuchukua mkondo wake”. Alisema
Katika hatua nyingine Bw.Mkeyenge amesema TASAC kama Shirika la Umma linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na Serikali, hivyo linatoa wito kwa Umma kuwa na subira wakati Tume inapoyafanyia kazi mashauri hayo.


“Ninapenda kuwafahamisha kuwa, TASAC ni taasisi ya Serikali inayosimamiwa na Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali, hivyo basi mashauri yake kisheria yanasimamiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na shauri hili”.Alisema Bw.Mkeyenge


Kwa upande wake Msemaji mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari maelezo Gerson Msigwa ametoa wito kwa wanaotumia mitandao ya kijamii kuacha kupotosha wananchi na kuwapa taharuki badala yake wafike katika ofisi za Taasisi husika au ofisi za msemaji mkuu wa Serikali.


"Nitoe wito kwa watu mbalimbali ambao wanatumia majukwaa ya mitandaoni wengine hata kwenye baadhi ya vyombo vya Habari, Unapokua na jambo ofisi za Taasisi zipo wazi nenda kwenye ofisi ukikwama huko njoo ofisi za Msemaji Mkuu wa Serikali nitakupatia majibu lakini tusiende kupotosha wananchi kwa Mambo ambayo hayana ukweli wowote".Alitoa wito Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa
 

Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: