Mkuu wa wilaya ya Lushoto mkoani Tanga, Kalisti Lazaro, amewataka wanawake katika kijiji cha Kizara, Kata ya Ubiri wilayani humo kupata mimba na kuijaza dunia kutokana na upatikanaji wa huduma za kiafya katika kijiji hicho.

Mkuu huyo wa wilaya aliyasema hayo jana Jumatatu Machi 27, 2023 alipokua akikabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya Sh6 milioni katika Zahanati ya Kijiji hicho ambao ulikua ni msaada kutoka kwa shirika moja lisilo la kiserikali.

“Wale mliokua mnasitasita kuzaa na kupata mimba, sasa pateni mimba sehemu ipo, muijaze dunia,” alisema Kalisti.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, Kalisti aliwapongeza wanakijiji kwa kujitolea kutoa nguvukazi na kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo.

“Mwaka jana tulizindua zahanati hii na vifaa vichache lakini leo ndugu zetu wa Improving Tanzania Fund (ITF) wameamua kutuongezea vifaa mdalimbali vikiwemo vifaa na kwa mahitaji ya zahanati hii, kila chumba kimepata mahitaji yake yanayostahili,” alisema Kalisti.

Aidha Kalisti aliwataka wafanyakazi katika zahanati hiyo kuvitunza vifa hivyo na kuwataka wakina mama wa eneo hilo kutojifungulia majumbani na badala yake kufika zahanatini hapo kwa usalama wa mama na mtoto.

Zahanati hiyo ambayo ilijengwa kwa juhudi za wananchi mwaka 2018 kabla ya kupata ufadhili mwaka 2019 kutoka kwa shirika hilo lisilo la kiserikali ilipokea vifaa tiba kutoka kwa shirika hilo jana vikiwemo vitanda na magodoro.

Share To:

Post A Comment: