Na Angela Msimbira OR-TAMISEMI

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amesema utunzaji siri za Serikali ni jambo muhimu huku akiwataka Wakuu wa Wilaya kuacha kutumiana nyaraka za Serikali kwa kutumia mitandao ya kijamii au barua pepe binafsi.

Akifungua Mafunzo ya Uongozi kwa Wakuu wa Wilaya Tanzania Bara leo Machi 13, 2023 kwa niaba ya  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi hao kuwachukulia hatua watumishi wazembe, wabadhirifu na wanaokwamisha miradi ya Serikali katika maeneo yao.

“Utunzaji siri za Serikali ni muhimu sana hususani katika kipindi hiki cha utandawazi na matumizi ya mitandao ya kijamii yawapasa mzingatie kuwa siri ndio uhai wa Serikali. Hivyo, ni lazima kudhibiti uvujaji wa siri za Serikali. Epukeni kabisa kutumia mitandao ya kijamii kama whatsapp, ama email binafsi kutuma nyaraka za Serikali’ amesitiza Dkt. Mpango.

Amewataka watoa mada kuhakikisha wanasisitiza kuhusu matumizi ya walinzi binafsi (bodyguards) na Waandishi wa Habari binafsi katika Ofisi za Umma kwa kuwa zipo taratibu za umma za kupatiwa wasaidizi hao.

Dkt. Mpango amewataka viongozi hao kuhakikisha wanasimamia   maadili, nidhamu na uwajibikaji wa watumishi kwa wananchi na kuepuka lugha za matusi na kujifanya miungu watu.

“Msiende kuwa Miungu watu, nendeni mkatende haki kwa wananchi na watumishi walio chini yenu. Wahudumieni wananchi kwa staha, sikilizeni kero zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati. Ninyi kama Viongozi mnapaswa kuongoza kwa mfano na kuweni makini wakati wote mnapozungumza na Umma, hakikisheni mnatumia lugha fasaha na nzuri.”amesema .

“Epukeni kutoa lugha ya matusi. Aidha, mienendo yenu na muonekano wenu mbele ya jamii uwe ni wa mfano, mienendo isiyofaa kama ulevi, ufuska, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya madaraka yenu, ufisadi, rushwa n.k. haiendani kabisa na dhamana au heshima ya Mkuu wa Wilaya.” 

Aidha, amesema kuwa Mkuu wa Wilaya anayetarajiwa na Serikali ni yule anayetenda  haki, mwaminifu/mnyoofu, mwadilifu, mwenye tabia njema na mchapakazi, hivyo amewakumbusha kuwa wao ndio walioshikilia mpini na fyekeo la Serikali.

Share To:

Post A Comment: