Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko ameongoza kikao kati ya Wizara na Kampuni za dmg events na Ocean Business Partners Tanzania ambazo zinashirikiana kuandaa Jukwaa la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania kwa waka 2023 kwa kushirikiana na Wizara.


Mkutano huo wa Kimataifa uliokuwa ukifanyika mwezi Februari ya kila mwaka, mwaka huu utafanyika tarehe 25-26 Oktoba, 2023 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Februari 18, 2023 jijini Dar es Salaam, Waziri Dkt. Biteko amewaeleza wawakilishi wa kampuni hizo kuwa, Wizara inatarajia kupata matokeo makubwa kutokana na mkutano huo kubwa likiwa ni kuitangaza ipasavyo sekta ya Madini kimataifa ili kuhamasisha uwekezaji kutokana na nchi ya Tanzania kubarikiwa kuwa na madini mengi yakiwemo ya kimkakati ambayo yanahitajika sana duniani kwa sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ocean Business Partners Tanzania Balozi wa Heshima Brazil- Zanzibar Abdulsamad Abdulrahmim ameipongeza wizara ya madini kwa kukubali kushirikiana na kampuni hizo binafsi kuandaa mkutano huo ambazo zimekua na uzoefu wa miaka mingi kuandaa mikutano ya kimataifa kupitia sekta mbalimbali za kiuchumi.

Amesema mbali ya mkutano huo kutarajiwa kuitangaza Sekta ya Madini, pia, itawezesha kuhamasisha uwekezaji na kuzalisha ajira kutokana na shughuli mbalimbali zitakazofanyika kipindi cha mkutano huo.




Share To:

Post A Comment: