Wakuu wa Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Kilimo zinazojishughulisha na undelezaji wa pembejeo za Kilimo Utafiti na uzalishaji na wawakilishi wao wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano kati ya Taasisi hizo na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katikaafla iliyofanyika Februari 9, 2023 mkoani Morogoro.

Na Calvin Gwabara, Morogoro.

CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Kilimo zinazojishughulisha na undelezaji wa pembejeo za Kilimo Utafiti na uzalishaji zimesaini mkataba wa mashirikiano ujulikano 'MoU. ambao utasaidia kuongeza ushirikiano katika utendaji wa Taasisi hizo na kuongeza ufanisi na tija katika kilimo nchini.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof.  Maulid  Mwatawala kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda alisema awali SUA ilikuwa iingie makubaliano hayo na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na Taasisi ya Uthibiti ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kwa ajili ya kupokea wanafunzi kwenye mafunzo kwa vitendo lakini baadae Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akaagiza ziongezeke na Tasisi zingine zote zilizo chini ya wizara yake.

“MoU hii haina lengo la kuhamisha majukumu ya Taasisi fulani ya kisheria kwenda kwenye Taasisi nyingine bali ni kusaidiana katika utekeelzaji wa majukumu ili kupunguza mzigo ambao ungewezwa fanywa na Taasisi mbili ukafanywa na Taasisi moja na kuielemea na kupelekea kuchelewesha matokeo tarajiwa kwa Jamii na Taifa”alisema Prof. Mwatawala.

Mwatawala amewataka wakuu wa Taasisi hizo kuteua kila Taasisi mtu ambaye atakuwa ni mratibu katika utekelezaji wa makubaliano hayo ili wasaidie yale ambayo watakubaliana kuyafanya kati ya Taasisi na Taasisi yaweze kufanyika kwa ufanisi na kupendekeza kuwepo kwa vikao mara mbili kwa mwaka kuangalia maendeleo ya utekelezaji wa makubaliano hayo ili kuchochea ufanisi wake.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru alisema ushirikiano huo utasaidia sana katika kuweka mipango ya pamoja ambayo itasaidia kutoa matokeo yenye mchango mkubwa kwa Taifa na kutafuta fedha na rasiliamali zingine za kuendeshea Taasisi hizo.

“Tunachokifanya leo ni kitu kizuri sana maana kwa mchanganyiko wetu katika fani mbalimbali na majukumu yetu ya kitaasisi tunaweza kuanzisha miradi ya pamoja ambayo italeta tija kwenye kilimo kwa kutumia Sayansi Teknolojia na Ubunifu tukaweza kutoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo na uchumi wa Taifa”alisema Ndunguru.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo wa TPHPA ameahidi kuhakikisha yale yote watakayokuwa wamekubaliana kuyetekeleza kupitia Taasisi yake watayatimiza kwa ufanisi na kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha makubaliano hayo yanafanikiwa na kuleta tija.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Dkt. Stephan Ngailo amesema Taasisi yake imekuwa ikishirikiana na baadhi ya Taasisi hizo kwenye nyanja mbalimbali lakini kwa makubaliano hayo mapya yanaongeza wigo wa ushirikiano na tija.

“Ushirikiano huu lengo letu kubwa la mwisho na kumfikia mtu wa mwisho ambaye ni Mkulima ambaye anaweza kuwa mdogo,wa kati au mkubwa na lengo la Waziri ni tija na kwa kufanya kazi kwa pamoja kwani  kutasaidia kuondoa kazi moja kufanywa na Taasisi nyingi (duplication) na kupunguza gharama kwa kuwa kazi hiyo ingeweza kufanya na tasisi moja na wote tukapata matokeo” alibainisha Dkt. Ngailo.

Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Stanford Chijenga alisema  kama wadau wa mbegu wamekuwa wakifanya kazi na Taasisi hizo kwa nyakati tofauti ikiwemo kupokea Wanafunzi wa SUA na katika masuala ya Mbegu kutoka (TARI) na (ASA) lakini sasa umefunguliwa mlango mkubwa zaidi wa ushirikiano ambao anaamini utasaidia kuinua kilimo.

“Kama walivyobainisha wakuu wengine wa Taasisi, sisi kama TOSCI tunaamini sasakwa kuunganisha Taasisi hizi zote zinazohusiana na kilimo kunakuwa na nguvu ngine ya ziada inaongezeka katika kuisaidia jamii. Maana huko nyuma wengi kwa kutofahamu taratibu za uthibiti wa ubora wa mbegu, walidhani kuthibiti ubora wa mbegu ni jukumu linalowachelewesha, na hii ni kutokana na kutokuwa na uelewa sana wa namna shughuli zinavyofanyika. Lakini kupitia ushirikiano huu naamini tutafanya kazi kwa karibu zaidi kusaidia wakulima wa nchi yetu kupata mbegu bora” alisema Chijenga. 

Akitoa salamu za Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) Dkt. Sophia Kashenge alisema wamefarijika sana kuwa sehemu ya mashirikiano hayo kwakuwa wamekuwa wakifanya kazi na Taasisi hizo kwa nyakati tofauti kabla ya makubaliano hayo lakini sasa baada ya makubaliano hayo anaamini ni mwanzo mwingine mzuri wa kuendelea kufanya kazi zaidi kwa umoja.

“Kwanza nitumie nafasi hii kuishukuru SUA kwa sababu sisi kama wazalishaji wa mbegu kuna maeneo mengi ambayo tumekuwa tukiona tunaweza kufanya kazi nao vizuri hasa katika uzalishaji wa mbegu kwani tunaamini SUA wanazo mbegu nyingi ambazo wamezitoa na bado hazijafika kwa wakulima kwahiyo kwa ushirikiano huu tunaweza kuzalisha mbegu kwa pamoja” alisema Kashenge.

Kashenge amewapongeza SUA kwa kuanzisha kozi ya kuzalisha wataalamu wa mbegu nchini kwakuwa awali walikuwa wakiwatumia watu kwanza kwa kuwajenga lakini baada ya ujuio wa kozi hiyo na Wahitimu wa fani hiyo kutaongeza ufanisi kwakuwa kulikuwa na pengo kubwa la wataalamu wa mbegu nchini.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Upande wa Utawala Fedha na Mipango Prof. Amandus Muhairwa amewaomba wakuu wa Taasisi hizo kushikamana kwa pamoja kutetea hoja na mambo mbalimbali yanayohusu Sayansi nchini badala ya kuwa na kauli za kupingana kwenye mambo yaliyo wazi kisayasi kwa maslahi binafsi au ya Taasisi zao.

“Naiona hii kama nafasi nzuri sana maana kwa sasa tunaogelea kwenye Bahari mbaya sana yani Sayansi inapingwa na watu walioshiba ambao wanaweza kutukataza kutumia Viuatilifu ( Dawa za kuua wadudu) lakini kwa jinsi tunavyozidi kuongezeka hatutaweza kuviepuka hivyo vitu na ikafikia wakitushinda watasema hata tusitumie mbolea lakini kwa umoja wetu tukisimama tutaifikisha nchi yetu mahali pazuri” alieleza Prof. Muhairwa.

Makubaliano hayo yamesainiwa kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Kilimo ambazo ni Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI),Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Taasisi ya Uthibiti wa Mbegu Tanzania (TOSCI),Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Udhibiti wa Viuatilifu (TPHPA) na Vyuo vya mafunzo ya Kilimo (MATI).


    Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) upande wa Taaluma Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Maulid Mwatawala (kulia) akitoa salamu za SUA na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Stanford Chijenga ambao ndio waratibu wa ushirikiano huo.

   Wakuu wa Taasisi hizo,  wakisaini mkataba huo wa mashirikiano (MoU)
Wakuu wa taasisi hizo na wawakilishi wao wakifuatilia maelezo na uwekaji saini wa mkataba huo.

Hafla ya kusaini mktaba huo ikiendelea.
Uwekaji saini wa mkataba huo ukiendelea

Hafla hiyo ikiendelea 
Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: