Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Ridhiwani Kikwete amemuagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara kuweka mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi na kuwapatia hati wakazi wa eneo la ekari 2,390 zilizotolewa na Mhe. Rais katika Bonde la Kiru Wilaya ya Babati mkoani Manyara.


Kikwete ametoa agizo hilo kwa Kamishna Bw. Joseph Batinamani wakati alipofanya ziara leo tarehe 12 Februari 2023 katika kijiji cha Kiru Dick halmashauri ya wilaya ya Babati mkoa wa Manyara.


Kadhalika Kikwete ametoa agizo hilo kutokana na mgogoro uliopo kati ya wakazi wa Kijiji cha Kiru Dick Valley wilayani Babati Mkoa wa Manyara na muwekezaji wa kampuni ya Hamir Estate Ltd inayojishughulisha na kilimo cha miwa ambaye ni wamiliki wa awali wa Mashamba hilo


Aidha, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliamua kumega ekari 2,390 ambazo zilikuwa zikimilikiwa kihalali na Kampuni ya Hamir Estate Ltd kwenye mwaka 1999 na kuwapa wananchi ili kumaliza mgogoro huo.


“Natoa maelekezo kwa Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Manyara kulitambua eneo hili na kuliwekea mpango wa matumizi ya ardhi. Tambueni maeneo ambayo yanafaa kwa shughuli za kilimo na shughuli za wananchi natambueni maeneo ambayo tutawapanga wananchi ambao ambao hawana kabisa mashamba” Amesema Kikwete.


Pamoja na maamuzi hayo Kikwete amewaonya wakazi wa eneo hilo kujiepusha na uvunjifu wa amani kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu ambavyo vimekuwa vikiendelea katika eneo hilo na badala yake amewataka kuonesha ushirikiano kwa muwekezaji kwa kuwa tayari ameishatoa ekari 2,390.



Naye Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Makongoro Nyerere amewataka wakazi wa eneo hilo kuwa nasubira wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais ili wananchi hao waweze kupangwa na kumilikishwa maeneo hayo na kupatiwa hati za umiliki wa ardhi.


“Ni kweli Mhe. Rais tayari ameishatoa eneo la ekari 2,390 lakini bado inabidi taratibu zifanyike kama ambavyo umeelekeza waweze kupangwa, kupimiwa na kupatiwa hati ili kila mmoja amiliki sasa eneo lake” Alisema Makongoro.



Bonde la Kiru ni eneo la bonde la ardhi lenye rutuba kuliko eneo lolote la kilimo katika Mkoa wa Manyara linalopatikana katika Wilaya ya Babati Vijijini takribani kilomita 12 kutoka Babati Mjini njia ya Babati -Arusha.


Kutokana na eneo hilo kuwa na rutuba sana limevutia wawekezaji wakubwa wengi wa kigeni na wenyeji wachache kwenye shughuli za kilimo hasa kilimo cha miwa toka enzi za Mjerumani na baadae Muingereza pamoja na mataifa mengine kama Urusi, Swedeni, Marekani kuanzia miaka ya 1930.



Kuanzia mwaka 1968 mpaka miaka ya mwanzoni ya 1970 Serikali ilitekeleza sera ya uanzishwaji wa Vijiji vya Ujamaa ambayo ilipelekea kuanzishwa kwa Vijiji vya Ujamaa ndani ya baadhi ya mashamba haya ya wawekezaji katika Bonde la Kiru ambayo yalikuwa yamevamiwa na hayajaendelezwa.


Hali hii ilipelekea kuibuka kwa migogoro mingi ya ardhi katika Eneo la Kiru Valley baada ya Serikali kutambua na kusajili baadhi ya Vijiji ndani ya mashamba kutokana na uhitaji mkubwa wa ardhi uliokuwepo kipindi hicho.


Ili kutatua migogoro hii ilionekana ni bora kufuta umiliki wa mashamba hayo ili mashamba haya yarejeshewe kwa Wananchi ambao ni Wakazi wa Kijiji cha Kiru Dick Valley.


Hata hivyo hata baada ya Serikali kuchukua hatua ya ufutaji wa mashamba hayo na kuwagawia wananchi bado hatua hiyo haikuweza kumaliza mgogoro huu wa ardhi kwani baadhi ya wanavijiji waliendelea kutaka ardhi zaidi hali iliyoendelea kuleta mivutano ya miaka mingi baina ya wawekezaji waliokuwa na mashamba hayo.


Hali hii ya mivutano iliendelea na hali ilikuwa mbaya zaidi ambapo mwaka 2011 kulitokea uvunjifu wa amani (vurugu) zilizosababisha uharibifu wa mazao, vifaa, makazi na hatimaye maisha ya mlinzi wa shamba la Kiru Valley Estate.


Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: