Na John Walter-Manyara

Mtu mmoja amefariki dunia na wengine Saba kujeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha basi la abiria walilokodi aina ya Toyota Coster yenye namba T.840-DRD iliyokuwa  ikitoka Msibani Musoma kwenda Arusha.

Ajali hiyo imetokea asubuhi siku ya jumamosi Februari 11, 2023 katika Kijiji Cha Singu kata ya Sigino barabara kuu ya Babati –Singida.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara George Katabazi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema chanzo ni mfumo wa breki wa gari hilo kufeli ikiwa kwenye eneo la kona kali na mteremko eneo la Logia  kisha kutumbukia Kwenye Korongo.

Katabazi amemtaja aliyefariki ni dereva wa gari hilo aliyetambulika kwa jina la Juma Kea Majembe na mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Manyara.

Kamanda Katabazi amesema ndani ya gari hilo kulikuwa na abiria 29 na kwamba majeruhi wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Manyara.

Kwenye Kona hiyo ya Logia miezi kadhaa iliyopita watumishi watatu wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Manyara walipoteza Maisha wakiwa kwenye majukumu yao.
Share To:

Post A Comment: