Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amewatunuku vyeti jumla ya wahitimu 39 wakiwemo wanaume 25 na wanawake 14 wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) katika Stashahada ya Teknolojia ya Madini ya Vito na Usonara.
Akizungumza Dkt. Biteko katika mahafali hayo ambapo amepewa heshima ya kuongoza Mahafali ya kihistoria ya kwanza ya Stashahada ya Teknolojia ya Madini ya Vito na Usonara ya TGC amewapongeza wahitimu wote waliotunukiwa Stashahada na pongezi kwa kituo hicho kwa kuwezesha wanafunzi hao kuhitimu masomo yao.
Amesema, lengo la Serikali la kuanzisha kituo hicho lilikuwa ni kutekeleza Sera ya Madini ya Mwaka 1997 kuhusu uongezaji thamani madini nchini kwa kutoa mafunzo ya uchongaji wa vinyago vya miamba.
Ameongeza kuwa, Serikali imesisitiza kuongeza manufaa yatokanayo na Sekta ya Madini kwa kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika kwa upana zaidi hapa nchini ili watanzania wanufaike na rasilimali hiyo.
“Ili kuongeza manufaa yatokanayo na rasilimali madini nchini, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika shughuli za madini na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji nchini,’’ amesema Dkt. Biteko.
Ameeleza kuwa, hatua zilizochukuliwa zimewezesha kuongezeka kwa shughuli za utafutaji madini, uchimbaji, uongezaji thamani madini, biashara za madini na kupanuka kwa biashara kutokana na shughuli za madini ha hivyo kusababisha watanzania wazawa kupata fursa za ajira na nafas iza kibiashara kupitia shughuli hizo.
Vile vile, amesisitiza kuwa uanzishwaji wa Kituo cha Jemolojia ni uwekezaji uliofanywa na Serikali katika elimu ili kuwajengea watanzania ujuzi ambao unawawezesha kuingia moja kwa moja kuajiriwa Serikalini au katika Sekta binafsi au kujiajiri.
Pia ameeleza Dkt. Biteko kuwa, Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan iliazimia kuimarisha utoaji wa mafunzo katika kituo cha TGC kwa kupanua miundombinu ya kituo itakayokidhi mahitaji ili kuzalisha wahitimu wengi na wenye ubobezi kwenye masuala ya uongezaji thamani madini ya vito na metali hapa nchini.
“Serikali ya awamu ya sita imetoa shilingi bilioni saba ambapo shughuli za utekelezaji wa ujenzi zinaendelea. Hatua hii ikikamilika itawezesha kituo kutoa mafunzo kwa kiwango cha kimataifa na hivyo kuwezesha madini yetu yanayozalishwa nchini kupata soko la ndani na nje ya nchi,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Akizungumzia changamoto amesema, Serikali inatambua uwepo wa changamoto katika tasnia hiyo kama vile mitaji kwa ajili ya uanzishwaji wa viwanda vya kusanifu madini au vifaa vya utambuzi maabara na hivyo inaendelea kutafuta wafadhili na wawekezaji kwa ajili ya kuanzisha viwanda hivyo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametoa onyo kwenye vituo vya ununuzi wa madini wilayani Kahama kusitisha mianya ya utoroshaji wa madini inayoendelea. Amemuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Madini kufuatilia suala hilo ili uchunguzi utakapomalizika hatua Kali zichukuliwe kwa wote wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) Daniel Kidesheni, amesema kuwa kituo hicho kimepata mafanikio makubwa ya kitaaluma na kuweza kuboresha mfumo wa utoaji mafunzo.
Amesema, mafunzo yaliyotolewa tangu kuanzishwa kituo hicho ni pamoja na kuanzishwa kwa mafunzo ya astashahada katika fani za sayansi ya madini ya vito (gemology), ukataji na ung’arishaji madini ya vito (lapidary) na usonara.
Aidha, kituo kitoa huduma kwa wadau wa madini katika utambuzi wa madini ya vito, ukataji wa madini ya vito, utengenezaji wa bidhaa za usonara na uchongaji wa tuzo kwa kutumia miamba
Mahafali hayo ya kwanza yamehudhuliwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Augustine Ollal, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Jemolojia Tanzania Dkt. George Mofulu, Kaimu Kamishna wa Madini Mavuruko Msechu, Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mrisho Gambo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) Samy Mollel, Watumishi wa TGC na Wakuu wa Taasisi.
Post A Comment: