Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) itatumia zaidi ya shilingi bilioni Saba (7,000,000,000) katika ujenzi wa daraja jipya la Berega wilayani Kilosa, Morogoro.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa Miradi iliyofanywa na Bodi ya Ushauri ya TARURA Mkoani Morogoro, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Florian Kabaka alisema kuwa ujenzi wa Daraja hilo utaleta manufaa makubwa kwa wananchi wa Berega na maeneo mengine waliokuwa wakipata taabu baada ya daraja la awali kuvunjika .

“ Daraja hili linagharimu zaidi ya shilingi bilioni Saba na nimoja kati ya madaraja makubwa kabisa ambayo TARURA inatekeleza ujenzi wake kwa kutumia fedha za tozo. Sisi kama Bodi tunaridhika na namna Mradi unavyoendelea ambapo tunaambiwa umefikia asilimia 72 na unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2023, “ alisema Mhandisi Kabaka. 

Aidha alieleza kuwa daraja hilo litaleta ukombozi mkubwa sana kwa wananchi wa Berega kwa sababu litawaunganisha na maeneo mengine kama Gairo, Dodoma na Tanga, pamoja na kuwarahisishia wananchi kufika Hospitali ya Wilaya ya Berega.

Naye Mhandisi Benjamini Maziku, kaimu meneja wa TARURA, Mkoa wa Morogoro alisema kuwa Daraja hilo litakapokamilika litakuwa ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi Berega na Wilaya ya jirani ya Kilindi kwa  sababu litakuwa na uwezo wa kupitisha magari ya aina yote hivyo kuwarahisishia usafiri na usafirishaji wa mazao.

“ Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha hizi za tozo kwa ajili ya kuwa hudumia wananchi hawa, sisi kama TARURA Mkoa tusingeweza kujenga daraja hili ambapo takribani bilioni Saba nukta tisa (Bl 7.9) zitatumika ambazo hapo awali kabla ya kuongezewa Bajeti na hasa fedha hizi za Tozo, hii ndiyo ilikuwa  bajeti ya Mkoa mzima ,sasa bajeti ya mkoa imeongezeka mpaka shilingi bilioni 26. Tunamshukuru sana Rais, “ alisema Maziku.

Kwa upande wake ndugu Michael Majoro, mkazi wa Berega alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo itakuwa ni faraja kubwa sana kwao Kwani itawaondolea matatizo mengi yaliyokuwa yakiwakabili hasa nyakati za mvua.

“Kwakweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea daraja hili, hapa Wapo waliokufa, mifugo kusombwa na maji, wamama kujifungulia ng’ambo ya pili kutokana na kushindwa kuvuka wakati hospitali ipo hapo karibu tu. Mheshimiwa hapa ametukomboa kwakweli tunaona hili ni daraja la kisasa kabisa na lipo juu,” Majoro. 

Mradi wa Ujenzi wa Daraja la Berega unahusisha ujenzi wa Daraja lenye urefu wa meta 140, barabara mkaribio za daraja mete 600 na maboresho ya barabara kutoka Berega kwenda Dumbalume kilometa saba(km 7) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.

Bodi ya TARURA inaendelea na ziara yake ya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na TARURA katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.

Share To:

Post A Comment: