Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Dkt. Charles Msonde akiongea wakati wa kuhitimisha kikao kazi kilichowakutanisha Kaimu Katibu Wasaidizi wa TSC (hawapo pichani) kutoka ofisi za Wilaya kilichofanyika hivi karibuni mjini Morogoro.Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama akitoa neno la kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Dkt. Charles Msonde wakati wa kuhitimisha kikao kazi kilichowakutanisha Kaimu Katibu Wasaidizi wa TSC kutoka ofisi za Wilaya kilichofayika hivi karibuni mjini Morogoro.Washiriki wa kikao kazi cha Makatibu Wasaidizi wa TSC kilichofanyika hivi karibuni mjini Morogoro wakisikiliza hotuba ya Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Dkt. Charles Msonde 


 Na Mwandishi wetu – Morogoro.

 Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) ngazi ya Wilaya wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Maafisa Elimu pamoja na Wathibiti Ubora wa Shule ili kuweza kutoa huduma bora kwa walimu huku wakitakiwa kuwafuata walimu shuleni badala ya kukaa ofisini kusubiri walimu wapeleke shida zao. 

 Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR – TAMISEMI), Dkt. Charles Msonde wakati wa kuhitimisha kikao kazi kilichowakutanisha Kaimu Katibu Wasaidizi wa TSC kutoka Wilaya zote za Tanzania Bara kilichofanyika mjini Morogoro.

 Dkt. Msonde amefafanua kuwa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha  walimu wanahudumiwa wakiwa shuleni, hivyo TSC, Maafisa Elimu na Wathibiti Ubora wa Shule wanatakiwa kufanya ziara shuleni siku tatu kila wiki na siku mbili pekee ndizo wanazotakiwa kubaki ofisini.

 “Serikali haitaki mwalimu aje kutafuta huduma ofisini kwako, ninyi ndio mnapaswa kwenda shuleni kutatua changamoto zao. Kuanzia sasa tumeachana na utaratibu wa zamani wa mwalimu kuja ofisini kupiga magoti akitafuta huduma. Tunataka mwalimu afanye kazi yake ya kufundisha tu, hayo mambo mengine ya madaraja, likizo, nk sisi tuliopewa dhamana ya kuwaratibu ndio tunatakiwa tuyafanye,” amesema Msonde.

 Kiongozi huyo ameongeza kuwa anatambua kuwa ofisi za TSC ngazi ya wilaya zinakabiliwa na changamoto ya vyombo vya usafiri, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kushindwa kutembelea walimu shuleni kwa kuwa Wathibiti Ubora wa Shule na Maafisa Elimu wana magari, hivyo amewataka kuhakikisha wanapanga ratiba ya kutembelea walimu kwa pamoja.

 “TSC, Maafisa Elimu na Wathibiti Ubora wa Shule lazima muelewe kwamba, shamba lenu ni kwa walimu ambao wapo shuleni. Hata kama kuna changamoto ya usafiri ni lazima tufanye kila linalowezekana kumfikia mwalimu alipo. Ndiyo maana tumeagiza maafisa elimu wote wanapopanga ratiba zao kwenda shuleni lazima ziendane na ratiba zenu ili mfanye ziara pamoja. Kila mmoja anatakiwa kujua kuwa ana mchango katika kuleta maboresho ya elimu katika Taifa hili, mmoja anaposhidwa kutekeleza wajibu wake maana yake ni kwamba tumeshindwa wote,” amesema. 

 Msonde amesisitiza kuwa hadhi na heshima ya mwalimu ni lazima ilindwe na ni marufuku kumnyanyasa mwalimu kwa namna yoyote ile kwani kufanya hivyo kunamwondolea morali ya kulea wanafunzi kiakili, kimwili, kiroho na kijamii na hivyo kutokea ongezeko la mmomonyoko wa maadili na maendendelo ya elimu kurudi nyuma.

 “Lazima tulinde hadhi ya mwalimu, sipendezi kuona au kusikia mwalimu ananyanyaswa. Ndo maana tumesema muwe shuleni kwa siku tatu kila wiki, ofisini tumewaachia siku mbili tu. Muende kuwatia moyo walimu wetu sio muende kukoroma kwa wakuu wa shule, hapana. Mnakwenda shuleni, mshirikiane nao professionally (kitaaluma), muwaone watoto darasani wana mapungufu gani na mkae na walimu kutafuta ufumbuzi kwa pamoja.” 

 Ameongeza kuwa, “Tunataka walimu wetu wajisikie kwamba ni watu wanaohudumiwa na walimu wenzao waliopewa dhamana ya kuwaratibu ili nao wajisikie kuwa ni watumishi wanaoheshimiwa,” amesema. 

 Naibu Katibu Mkuu huyo alihitimisha kwa kusema kuwa kufanya kazi kwa bidii na kujituma ni moja ya njia za kuunga mkono juhudi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kipindi kifupi alichokaa madarakani amefanya mapindizi makubwa katika sekta ya elimu nchini.

 “Rais amefanya mambo mkubwa katika kuleta mapinduzi ya elimu, kwa miaka 5 kuanzia mwaka 2021 kiasi cha shilingi trilioni 1.2 kinaendelea kutumika kujenga shule 1026 za Sekondari. Kwenye shule za Msingi kupitia Mradi wa BOOST kiasi cha shilingi trilioni 1.15 zitatumika kwa ajili ya kuimarisha elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya, ukarabati wa shule, ujenzi wa madarasa,  pamoja na kuendeleza utumishi wa walimu ambapo TSC ni miongoni mwa wanufaika katika mradi huo.

 Naye Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Paulina Nkwama amesema kupitia Mradi wa BOOST TSC imeweza kufanya mapitio ya Ufafanuzi wa Kanuni za Maadili na Utendaji Kazi katika Utumishi wa Walimu ambapo imeandaa kitabu cha ufafanuzi huo kitakachosambazwa shuleni ili kuwafanya walimu watekeleze wajibu wao kwa kuzingatia miiko na taratibu za kazi hiyo.

 Amesema kikao kazi hicho kilichofanyika kwa siku nne kuanzia Januari 24 – 27, 2023 pamoja na mambo mengine, kilikuwa cha mafunzo kwa Kaimu Katibu Wasaidizi 139 wa kuhusu ufafanuzi wa Kanuni hizo ambao nao watakwenda shuleni kutoa elimu hiyo kwa walimu.

Share To:

Post A Comment: