Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akiwahutubia watu wasioona ambao wameshiriki mafunzo maalum ya usalama na afya jijini Dodoma. Waziri huyo alikuwa anafungua mafunzo hayo pamoja na kuzindua kitabu chenye maandishi ya nukta nundu ambacho OSHA imekiandaa kwa ajili ya kufundishia kundi hilo.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akitoa maelezo ya awali kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa kitabu maalum cha mafunzo ya Usalama na Afya kwa watu wasioona.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akimkabidhi fimbo nyeupe mmoja wa washiriki wa mafunzo ya usalama na afya kwa watu wasioona. Fimbo hizo zilitolewa na OSHA kwa washiriki wa mafunzo hayo ili kuwawezesha kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine bila changamoto.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (wapili kushoto), akiwa katika meza kuu na viongozi wengine wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usalama na afya kwa wasioona pamoja na uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (katika), Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Yahaya Massare (wakwanza kulia), Mtendaji wa OSHA, Khadija Mwenda (wapili kulia), Mkurugenzi wa Watu Wenye Ulemavu-Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Rashid Maftah (wakwanza kushoto) na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB), Bw. Omary Itambu- wakionesha kitabu cha masuala ya Usalama na Afya kilichoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu mara baada ya kitabu hicho kuzinduliwa na Waziri Prof. Ndalichako.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akimkabidhi kitabu cha masuala ya Usalama na Afya kilichoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu mmoja wa washiriki wa mafunzo ya usalama na afya kwa watu wasioona.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akisalimiana na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya usalama na afya kwa watu wasioona ambayo yametolewa na OSHA katika Mkoa wa Dodoma.


Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya usalama na afya kwa watu wasioona wakifuatilia mada mbali mbali zilizowasilishwa na wataalam kutoka OSHA.Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umezindua kitabu maalum cha mafunzo ya usalama na afya kwa ajili ya watu wasioona ambacho kimeandikwa kwa maandishi ya nukta nundu ili kuliwezesha kundi hilo kujifunza kanuni bora za usalama na afya katika shughuli zao za kila siku.

Kitabu hicho kimezinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako jijini Dodoma mbele ya wawakilishi 100 wa watu wasioona kutoka Mkoa wa Dodoma ambao wamepatiwa mafunzo ya siku moja ya usalama na afya kwa kutumia kitabu hicho.

Akizindua kitabu sambamba na kufungua mafunzo hayo, Waziri Ndalichako, amewataka watu hao wasioona kutumia kitabu hicho kwa malengo yaliyokusudiwa na serikali ambayo ni kuwapa nyenzo ya kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kuzingatia taratibu muhimu za usalama na afya.

“Ndugu washiriki nimefuraha kuona kwamba OSHA leo wameandaa mafunzo haya lakini jambo la muhimu zaidi katika mafunzo haya ni kwamba wameandaa kitabu maalum kilichoandikwa kwa maandishi ya nukta nundu ambayo watu wasioona wanaweze kusoma na kuelewa maudhui yaliyomo katika kitabu hicho,” amesema Prof. Ndalichako.

Aidha, Waziri huyo mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi amesema serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha huduma mbali mbali za watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutunga Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbali mbali ili kuhakikisha kuwa ustawi wa watu wenye ulemavu unazidi kuimarika.

“Pamoja na kuipongeza Taasisi OSHA kwa kutambua umuhimu wa kuandaa chapisho hili kwa kushirikiana na viongozi wa vyama vya wasioona, niwaagize kuchapisha nakala za kutosha na kuzisambaza kwa makundi mengine zaidi sambamba na kuendelea kutoa mafunzo hayo muhimu sana kwa kila mfanyakazi kutegemeana na shughuli anazozifanya,” ameeleza Prof. Ndalichako.

Waziri Ndalichako ameongeza kuwa kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina watu wapatao 61,741,120 na uchakataji wa matokeo hayo kwa makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu unaendelea kukamilishwa ambapo utawezesha kupata idadi kamili ya watu wenye ulemavu na hivyo kurahisisha utoaji wa huduma mbali mbali kwa kundi hilo muhimu katika jamii.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema wameandaa chapisho hilo na mafunzo tajwa ikiwa ni utekelezaji wa jukumu la Taasisi linalowataka kutoa elimu ya usalama na afya kwa makundi mbali mbali katika jamii wakiwemo watu wenye ulemavu.

“Sisi kama OSHA tunatambua kwamba ulemavu ni hali tu ambayo hawaondolei utu watu wenye ulemavu wala nafasi yao ya kushiriki katika shughuli mbali mbali za kiuchumi hivyo tunayo programu maalum ya kuyawezesha makundi mbali mbali wakiwemo watu wenye ulemavu kufanya kazi zao za kila siku katika hali ya usalama na afya,” amesema Mwenda na kuongeza:

“Hivyo tumekuwa tukitoa mafunzo kwa makundi mbali mbali wakiwemo wachimbaji wadogo, wakulima, mama lishe, mafundi pamoja na watu wenye ulemavu kama tutakavyofanya kwa kundi hili la watu wasioona ambalo tumekwenda mbali zaidi kwa kuwaandalia kitabu maalum cha mafunzo.”

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania, Bw. Omary Itambu wameishukuru Taasisi ya OSHA kwa kutilia mkazo suala la uwezeshaji wa watu wenye ulemavu hususan wasioona.

“Tunaishukuru Taasisi ya OSHA kwa jitihada inazofanya katika kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma katika masuala haya ya usalama na afya. Nasi tunaahidi kuitumia vema nafasi hii ambapo tutayazingatia yote wanayotufundisha na hivyo kuweza kuzalisha kwa tija kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu,” amesema, Omary Itambu, Mwenyekiti Jumuiya ya Wasiona Tanzania.

“Tunashukuru kwa kupatiwa vitabu hivi vyenye maandishi ya nukta nundu pamoja na mafunzo mazuri tuliyopatiwa na tunaahidi kwenda kuwafundisha na wenzetu ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo,” ni maneno ya Lucy Amri Bupamba, mshiriki wa Mafunzo.

Uzinduzi wa kitabu hicho umefanyika sambamba na mafunzo ya siku moja kwa watu wasioona 100 wa Mkoa wa Dodoma kwa kutumia kitabu hicho. Aidha, OSHA imetoa msaada wa fimbo nyeupe kwa washiriki wote kwa ajili ya kuwasaidia kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: