WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maboresho yaliyofanyika katika hospitali ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Oktoba 18, 2022 alipofanya ziara hospitalini hapo.

 

Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara katika hospitali hiyo na alieleza kutorishwa na milango iliyowekwa na kuagiza iondolewe na iwekwe mingine yenye viwango na leo Januari 06, 2023 amekagua maendeleo ya utekelezaji wa agizo na ameridhishwa na kazi iliyofanyika.

 

Kufuatia utekelezaji huo Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na utekelezaji wa maelekezo hayo ambapo hadi sasa jumla ya milango 67 kati ya 84 imeondolewa na kuwekwa mipya yenye ubora.

 

“Leo nimeona milango bora kabisa, kwa nini tulikubali kuweka milango mibovu wakati mizuri ipo? Hii haikubaliki kwa sababu tunapoteza fedha za Serikali zinazotokana na kodi ya wananchi. Ni lazima kila mtumishi wa umma atimize wajibu wake.”

 

Amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya ili kusogeza huduma muhimu za kijamii karibu na wananchi.

 

Pia, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Idara katika halmashauri zote nchini wasimamie kikamilifu utekelezaji wa shughuli zote za maendeleo katika maeneo yao ili kuhakikisha fedha zinazoidhinishwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi zinatumika ipasavyo.

 

“Haipendezi kuona viongozi wakuu waje na kubaini madudu katika miradi wakati watendaji mpo. Kila mtumishi awajibike ipasavyo katika eneo lake ili kuhakikisha lengo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia la kuwaletea maendeleo wananchi linatimia.”

 

Mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 7.5, mpaka sasa hospitali hiyo imepokea shilingi bilioni 4.2 kutoka Serikali kuu ambapo majengo 20 yameshajengwa, majengo 13 yamekamilika, majengo saba yapo katika hatua za ukamilishaji. Hospitali itakapokamilika inatarajia kuhudumia watu Zaidi ya 200,000.

 

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuiboresha sekta ya afya ikiwemo kununua magari mawili kwenye halmashauri zote 184 nchini ikiwa moja nila wagonjwa na linguine ni kwa ajili ya usimamizi wa huduma za afya.

 

Akizungumza kuhusu ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Namtumbo, Dkt. Dugange amesema watahakikisha wanasimamia maagizo  yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu ili kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati na inaanza kudahili wanafunzi

 

Awali, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Christopher Wabarumi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na wilaya hiyo ambayo inaendelea na ujenzi wa majengo ya 22 katika hospitali ya wilaya hiyo.

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Januari 6, 2023 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

 

Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya shilingi bilioni 4 kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), awamu ya kwanza ilianza April 2022 na inaotarajiwa kukamilika Januari 30, 2023 ambayo itagharimu shilingi bilioni tatu. Shule hiyo itakapokamilila itapokea wanafunzi 1,080 ambapo awamu ya kwanza itapokea wanafunzi 600.

 

Awamu ya kwanza imehusisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo mabweni matano, bwalo, vyumba 12 vya madarasa, jengo la utawala, nyumba ya mwalimu, mfumo wa maji safi na maji taka, vyoo matundu 16, uzio, kichomea taka, chumba cha jenereta na njia za kutembelea.

 

Aidha, awamu ya pili ambayo ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu kwa gharama ya shilingi bilioni moja  itahusisha ujenzi wa madarasa 10 yenye ofisi za walimu tatu, chumba cha ICT, Maktaba, nyumba nne za walimu na mabweni manne.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwaRais Mheshimiwa Dkt. Samia ameamua kuwekeza kwenye elimu ya mtoto wa kike kwa kujenga shule za wasichana nchi nzima ili kumpunguzia changamoto zilizokuwa zikimkabili. “Si kwamba amemtenga mtoto wa kiume hapana, ameamua kwenda nao wote.”

 

Pia, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wanaojenga shule hiyo kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa ili waanze kupokea wanafunzi. Shule ya Sekondari  Dkt. Samia Suluhu Hassan inatarajia kuanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano Julai, 2023.

Share To:

Post A Comment: