Na John Walter-Manyara

Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Manyara kimepongeza hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu kufanyika kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini iliyokuwa imezuiliwa kwa muda mrefu.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Manyara Toima Peter Kiroya, amesema kuwa wanampongeza Rais Samia kwa ruhusa mikutano hiyo huku wakiahidi kufanya siasa safi  kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.

Kiroya amesema hatua hiyo inaondoa manung’uniko yaliyokuwepo na hivyo kutoa nafasi kwa wananchi kupata nafasi ya kushiriki na kuendeleza amani, umoja na mshikamano wa taifa la Tanzania kwa lengo la kujiletea maendeleo.

Ameongeza kuwa  “Sisi wanachama wa chama cha Mapinduzi na wananchi wa mkoa wa Manyara tunaahidi kwa Mheshimiwa Rais na Seriakali yake kuwa tutatekeleza maamuzi na maelekezo yake kwa vitendo na kuzingatia taratibu, sheria na kanuni zinazoongoza sheria hii.

Aidha chama hicho mkoa wa Manyara kimempongeza Rais Samia kwa dhamira yake ya dhati kupitia serikali  wa kukwamua mchakato wa marekebisho ya katiba.

Uamuzi huu unaonyesha wazi kuwa Rais Dr. Samia Suluhu Hassan anatekeleza kwa vitendo mapendekezo ya kamati ya maridhiano, kamati ambayo aliiunda yeye mwenyewe kwa ridhaa ya chama cha mapinduzi” alisema Kiroya

Nao baadhi ya  wananchi wa Mjini Babati wamempongeza Rais Dkt.Samia wakisema  ruhusa hiyo itaonyesha ukomavu wa kisiasa pamoja na kusaidia kuibuliwa kwa changamoto nyingine zilizojificha kupitia vyama vya kisiasa .

Share To:

Post A Comment: