NA FARIDA MANGUBE - MOROGORO.

Katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunza katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya kimemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kuzungumza na mawaziri watano wanaodaiwa kumiliki mifugo mingi katika Wilaya hiyo ili waiondoe haraka na kunusuru vyanzo vya maji.

Akizungumza kwenye ziara ya Waziri wa Maji Jumaa Uweso wakati akizindua ujenzi wa miundombinu ya mradi wa maji katika kata na Kijiji cha Lundi Mwenyekiti CCM Wilaya ya Morogoro Gerold Mlenge alisema kiasili wilaya hiyo haina eneo la ufagaji bali ni kilimo lakini kwa sasa kuna wafugaji wengi kuliko wakulima ambao ni wavamizi na kuwasumbua wakulima huku wakiharibu vyanzo vya maji.

Mlenge alimuomba Waziri Aweso kuchukua majina ya mawaziri hao kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Albert Msando ambaye tayari ameshafikishiwa taarifa na majina hayo na kuahidi kuyafanyia kazi

“sasa isifike mahali nikaita press nikawataja kwa majina, muende mkanongonezane watoe, huku Morogoro vijijini hatuna asili ya mifugo, sisi kazi yetu ni kulima, hatutaki migogoro, hatutaki migogoro ya wakulima na wafugaji” alisema.

Akizungumza na wananchi kwenye Kijiji cha Lundi Waziri wa maji Jumaa Aweso alisema changamoto ya maji hasa kuharibika kwa vyanzo vyake zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara zinazoshabihiana na suala la mifugo ambapo aliahidi kuliwasilisha lalamiko lao la mawaziri watano wanaomiliki mifugo wilayani humo kama lilivyo kwa Rais bila kukosa

“nimepewa ombi maalum na viongozi hapa, juu ya changamoto ya mifugo, nikiri kulipokea na nitalipeleka kama lilivyo kama mlivyotaka, mimi ni muathirika pia, moja ya changamoto kubwa sana ni kuharibika kwa vyanzo vya maji, hivyo nitaliwasilisha sababu hata kule kwenye uzinduzi wa bwawa la Nyerere Mheshmiwa Rais alieleza uelekeo na nitalifikisha ili kuhakikisha jambo hilo linapata ufumbuzi” alisema Waziri Aweso.

Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa miundombinu ya mradi wa maji Lundi Meneja wa RUWASA Wilayani humo Mhandisi Grace Lyimo alisema mradi huo unagharimu kiasi cha sh mil 492.8 ambao ukikamilika kwa asilimia 100 utatimiza azma ya Serikali ya awamu ya sita ya kutoa huduma bora za maji kwa wananchi 4604 wa vijiji vya Ng’ongola na Lundi kwenye vitongoji saba.

Alisema mradi huo umeanza kutekelezwa tangu Januari 17 mwaka 2022 na ulitarajiwa kukamilika Julai 16 mwaka 2022 ambapo umeongezewa muda na kutakiwa kukamilia Februari 7 mwaka 2023 kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza.

Alisema chanzo cha maji cha Mradi huo ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 264,000 kwa siku na mahitaji ya maji katika vijiji hivyo viwili ni lita 230,200 kwa siku.

Lyimo alifafanua kuwa kazi kuu zilizopangwa katika mradi huo ni ujenzi wa tenki la lita 150,000, ujenzi wa nyumba mbili za mitambo ya kusukuma maji, kunganisha umeme wa Tanesco, kazi ya kuchimba, kulaza bomba na kufikia urefu wa kilomita 19, ununuzi wa bomba za laini kuu na bomba za kusambaza maji, kujenga vituo 17 vya kuchotea maji vijijini na ukarabati wa vituo sita vya maji.

Aliataja kazi zingine kuwa ni ukarabati wa matenki mawili yam aji na ujenzi wa ofisi ya jumuiya za maji na ununuzi wa pikipiki mbili kwa ajili ya usimamiz na uendeshaji wa mradi utakapokamilika.

Alisema kwa ujumla utekelezaji wa kazi katika mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 69 na kiasi cha sh mil 212.5 kimeshalipwa kwa mkandarasi

Kwa upande wao wananchi walionufaika na mradi huo akiwemo Bi. Rehema Hembela alimshukuru Rais Samia kwa kupeleka mradi huo wa kumtua mama ndoo kichwani utakaowasaidia watu wanaochota maji mbali na wengine wanaotumia maji yasiyosalama hasa vijiji vya Kisaga na Vihengele ambao wanakunywa maji yasiyo safi na salama.
Share To:

Post A Comment: