Wakulima wa mikoa ya Songwe na Mbeya, wanalalamikia kitendo wanachodai kuwa baadhi ya mawakala wanaficha mbolea ya ruzuku, hali inayowaletea usumbufu mkubwa.

Baadhi ya wakulima mkoani Songwe, wanadai kuwa wapo baadhi ya mawakala hao walioanza kulangua mbolea ya kukuzia aina ya UREA kwa kuwauzia bei ya Sh90,000 badala ya Sh70,000 iliyotangazwa na Serikali.

Mwananchi jana lilishuhudia foleni kubwa ya wakulima waliofika kununua mbolea hiyo kwenye moja ya duka la wakala wilayani Mbozi mkoani Songwe.


Baada ya kuzungumza nao, walionyesha hofu ya kuwapo kwa mtiririko mdogo wa uingiaji wa mbolea ambao umekuwa chanzo cha kupata watu wachache.

Mmoja wa wakulima hao, John Nzunda alisema ni zaidi ya wiki moja sasa kumekuwa na uhaba wa upatikanaji mbolea, hali iliyosababisha kuzuka kwa walanguzi ambao wanauza mbolea hiyo ya ruzuku aina ya UREA kwa bei ya Sh90,000 tofauti na ile iliyotangazwa na Serikali ya Sh70,000.

“Tunahisi kuna ujanja, maana tukienda kwa mawakala wengi hawana mbolea matokeo yake tumekuwa tukiahidiwa na kupewa majibu ya kusubirishwa,” alisema Nzunda.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha wakulima na Wafanyabiashara (TCCIA) mkoani hapa, Charles Chenza alisema chanzo cha kukosekana kwa mbolea kinatokana na mgawanyo mbovu hivyo kusababisha ulanguzi.

Ofisa Kilimo wilayani Mbozi, George Nipwapwacha alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima na kuwataka kutoa taarifa ofisi za Serikali wanapowabaini walanguzi wa mbolea hiyo badala ya kulalamika tu.

“Ni kweli, kwa wiki moja sasa mbolea ya UREA ipo chache wilayani hapa,” alisema.

Alisema tangu Desemba 27, kampuni ya Export Trading General (ETG, imeshapeleka tani 11,000 za mbolea ya UREA. Hata hivyo, aliwaondoa hofu wakulima hao kuwa kampuni nyingine zitaendelea kupeleka mbolea hiyo muda mfupi ujao.


Mkoani Mbeya

Baadhi ya wakulima mkoani hapa nao wamelalamikia kuadimika kwa mbolea ya ruzuku.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti walisema tangu mbolea hiyo ilipofikishwa kwa mawakala, haipatikani.

Mkulima, Faustina Charles alisema: “Mfumo wa ununuzi kwa kutumia namba pia ni changamoto, unakuta namba yako imefika zinaanza sababu kutolewa kwa wakala mara mbolea imekwisha mara mtandao wa kuwaingiza kwenye mifumo iko chini, ni usumbufu juu ya usumbufu.”

Mkulima mwingine, Charles Michael ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia kupata mbolea hiyo sasa, kwa kuwa muda wa kuitumia umeshawadia.H.T : Mwananchi

Share To:

Post A Comment: