Naibu Waziri wa Maji ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya Mhandisi Maryprisca Mahundi amekabidhi vifaa vya tehama shule ya msingi Iwambi ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoahidi mwaka jana katika zoezi la upandaji miti lililoongozwa na kikundi cha Iwambi Active Group chini ya Mwenyekiti wake Melania Kifaru.


Mahundi amesema amewiwa kutoa vifaa hivyo kwa lengo la kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akitoa fedha nyingi katika sekta ya elimu ikiwemo ya ujenzi wa madarasa shule za msingi na sekondari.


'Mimi kama Mbunge nitahakikisha nasaidia sekta ya elimu ili wazaliwe kina Marprsca wengi na kina mama Samia wengi'alisema Mahundi.


Hata hivyo Mahundi amewataka wananchi kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya maji,barabara,afya na elimu.


Akipokea vifaa hivyo Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Iwambi Eliah Kasanga amesema vifaa hivyo vitasaidia kutunza nyaraka za shule sambamba na kudurufu mitihani ambayo walikuwa wakichapa mitaani.


Kwa upande wake Gilbert Kasebele mratibu wa elimu Kata ya Iwambi amesema shule nyingi katika Kata yake zina changamoto nyingi hivyo Mahundi asichoke kusaidia pindi atakapoombwa.


Diwani wa Kata ya Iwambi Humphery Ngalawa amemshukuru Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi kwa moyo wake wa kusaidia shule katika Kata yake na kutoa wito kwa wadau wengine kujitolea kutatua changamoto mbalimbali hususani za elimu.


Mwenyekiti wa Iwambi Active Group Melania Kifaru amesema Mhundi ni mkazi wa Iwambi hivyo msaada wa vifaa vya tehama vitachangia maendeleo katika kata hiyo ambapo mwaka jana walipanda miti katika taasisi zote zilizopo Kata ya Iwambi.

Share To:

Post A Comment: