Na John Walter-Manyara

Mkuu wa Usalama Barabarani mkoa wa Manyara SSP Georgina Matagi amewataka madereva  na wamiliki wa mabasi ya abiria yaendayo maeneo mbalimbali ya  mkoa huo na nje pamoja na wamiliki na madereva wa mabasi madogo ya abiria maarufu kama daladala kuhakikisha wanafanya  ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara katika magari yao ili kupunguza ajali zinazosababishwa na ubovu na uchakavu wa magari.

Ameyasema hayo wakati alipofanya ukaguzi wa kushtukiza  katika kituo Kikuu cha mabasi mjini Babati  kwa lengo la kuangalia hali ya usalama wa kituo hicho,  kuona namna madereva wanavyotii sheria za usalama barabarani kwa kuzingatia ubora wa vyombo wanavyoviendesha.

Aidha, amewataka  wananchi  kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa taarifa pindi wanapoona dereva anavunja sheria kwa kuendesha mwendo kasi  na kutoa wito kwa  wamiliki wa magari, madereva pamoja na abiria kufuata na kuheshimu sheria na kanuni za usalama barabarani ili kuepuka makosa na ajali za barabarani.

Kwa upande wake meneja mfawidhi wa LATRA mkoa wa Manyara Joseph Michael amewakumbusha madereva pamoja na wapiga debe kuwakatia wateja wao tiketi mtandao kama taratibu zinavyoelekeza.

 

Naye mwenyekiti wa madereva mkoa wa Manyara na Arusha Loi Lotti amesema hatua hiyo ya ukaguzi ni nzuri kwa kuwa inawakumbusha madereva wajibu wao huku akiomba jeshi la polisi linadhibiti waendesha Power Tiller majira ya usiku kwa kuwa zimekuwa chanzo cha ajali nyingi Magugu.

Share To:

Post A Comment: