Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka Maafisa Habari/ Uhusiano na Mawasiliano wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza kasi ya kutangaza vivutio vya utalii ili kuifungua Dar es Salaam kiutalii.


Hatua hiyo ni kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tour.

Mhe. Mary Masanja ameyasema hayo leo mara baada ya kukutana na Maafisa Habari katika kikao kazi kilichofanyika kwenye Ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) jijini Dar es Salaam.

Mhe. Masanja amesema ni lazima kuifungua Dar es Salaam kiutalii kwa kuwa ndio lango kuu la kupokelea wageni kutoka nchi mbalimbali duniani.

“Lazima kila mwezi tuwe na tukio la kiutalii jijini Dar es Salaam na tufanye kwa kushirikiana”.

Aidha, amesema ni jukumu la kila taasisi kuhakikisha inatangaza vivutio vyote bila kubagua taasisi nyingine.

“Taasisi zote za Wizara ya Maliasili na Utalii zinatunza, zinahifadhi na zinaendeleza utalii hivyo tunachotakiwa kufanya ni kumuunga mkono Mheshimiwa Rais ili kile alichokianzisha kilete matokeo chanya.”Mhe. Masanja amesisitiza.

Amewataka maafisa hao kutenga bajeti za kutangaza vivutio vya utalii vya maeneo yao ya kazi kupitia vipeperushi na kuviweka katika maeneo yanayotembelewa na wageni.

“Vipeperushi vinatakiwa vionekane katika maeneo yote ambayo watalii wanafika hapa jijini Dar es Salaam kama hoteli, viwanja vya ndege na magari yanayobeba abiria “madereva taxi” wanaopokea watalii ili kuvutia watalii wengi zaidi. Vipeperushi hivyo viwe na vivutio vyote vya utalii vya maeneo yote ya taasisi za Wizara ambazo ni TAWA, TANAPA, TFS na MAKUMBUSHO YA TAIFA.

Sambamba na hilo amezitaka taasisi za Wizara hiyo kuitumia fursa ya meli inayoleta watalii nchini kwa kutangaza ujio wake kwa kualika waongoza watalii kushiriki katika kuwapokea na kuwatembeza katika vivutio mbalimbali vilivyoko jijini Dar es Salaam.

Mhe. Masanja amehitimisha kikao hicho kwa kuwataka maafisa hao kuisemea Wizara kwa nguvu moja ili kufikia malengo ya kuongeza idadi ya watalii nchini.
Share To:

Post A Comment: