Serikali imetoa rai kwa vyuo vyote nchini vinavyo fundisha fani za uhasibu, fedha, uchumi na biashara kuhusisha Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwa na wataalamu watakao simamia vyema mifumo ya fedha na kuondoa vihatarishi vilivyopo.


 Rai hiyo imetolewa Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Bw. Athumani Mbuttuka wakati wa mahafali ya 24 ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), jijini Arusha.


 Bw. Mbutuka alisema kuwa mapato mengi yanakusanywa kupitia mifumo hivyo wahasibu wenye utaalamu wa Tehama wanaweza kuhakikisha kuwa mifumo hiyo ya kifedha inakuwa salama.


“Wahasibu wengi wanaweza kufanya uchambuzi mzuri wa data lakini tunauhitaji wataalamu wa uhasibu na Tehama ili kufanya kazi kwa ufanisi na kuhakikisha kunakuwa na usalama zaidi katika mifumo ya mapato hususani kwa kudhibiti wanaofuta taarifa za mapato kutoka kwenye chanzo”, alisema Bw. Mbuttuka.


Alisema kuwa vyuo vinavyotoa fani za Tehama vihakikishe masuala ya ukaguzi na fedha unakuwa sehemu ya fani hiyo ili kuondoa vihatarishi katika maeneo hayo jambo linaloweza kuongeza ajira nyingi kwa kuwa eneo la ukaguzi kunauhaba mkubwa.

Bwana Mbuttuka alisema kuwa wakati Kenya inawataalamu wa ukaguzi wa mifumo ya taarifa waliothibitishwa 1456 Tanzania walikuwa 152, hadi Novemba, 2021 hali ambayo inaashiria kuwa Chuo cha Uhasibu Arusha na Vyuo vingine vya aina hiyo vina  fursa ya kutoa wahitimu wengi zaidi wa fani hiyo na kukuza ajira nchini.

 Aidha Bw. Mbuttuka amekitaka Chuo cha Uhasibu Arusha kuhakikisha wataalamu wanaoandaliwa wanakuwa mstari wa mbele katika kutoa majawabu kwa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii, ili  kuchangia katika kujenga uchumi wa nchi na wa mtu mmoja mmoja.

Alisema Serikali imeandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025. Miongoni mwa Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ni pamoja na Kujenga Uchumi imara na wenye uwezo shindani na kuwaletea wananchi maisha bora.

 Alisema imani ya Serikali kwa Taasisi za Elimu ya Juu ni kuona mnaisaidia katika kutimiza malengo hayo ili kuboresha viashira muhimu vya kuendeleza sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii

Pia amekipongeza chuo hicho kwa usimamizi mzuri wa fedha za umma hususani katika ujenzi wa majengo mbalimbali ikiwemo madarasa, maabara za kompyuta, hosteli na majengo ya utawala ambayo yanajengwa kwa kutumia mapato ya ndani kupitia ‘force account’.

Alisema utekelezaji wa miradi hiyo umezingatia viwango vya ubora na thamani ya fedha, jambo ambalo ni la mfano na linapaswa kuigwa na Vyuo vingine, hivyo Wizara ya Fedha na Mipango imewaunga mkono kwa kuwaongezea fedha za miradi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Mwamini Tulli, ametoa rai kwa wahitimu kuhakikisha wanachangia katika uchumi wa nchi kwa kuwa Taifa linawahitaji.

Alisema kuwa Chuo kimewapa elimu ya nadharia na vitendo hivyo wasitegemee ajira za Serikali pekee kwa kuwa mafunzo waliyoyapata chuoni hapo yanawawezesha kufanya mambo mbalimbali, jambo la kuzingatia ni kujiamini kwa kuwa uwezo wanao.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha Dkt. Cairo Mwaitete, amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani, kwa kukipatia chuo hicho  Fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kiasi cha shilingi bilioni 44. Kwa ajili ya kuboresha miundombinu na elimu ili iendane na ulimwengu wa kisasa

Alisema fedha hizo zitatumiwa na Kampasi Kuu ya Arusha, Manyara na nyingine zitatumika katika Kampasi mpya inayojengwa Songea Mkoani Ruvuma.  

Katika mahafali ya 24 ya Chuo cha Uhasibu Arusha jumla ya wahitimu 3529 wamehitimu mafunzo yao katika ngazi mbalimbali ikiwemo Astashahada na Shahada za Uzamili, ambapo kati yao wanaume ni 2041 na wanawake ni 1488.












Share To:

Post A Comment: