Na John Walter-Manyara

 

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Paulina Gekul amewataka wananchi kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya zao na kuepuka maradhi mbalimbali yanayotokana na mtindo wa Maisha.

 

Amesema jamii isipokuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara ni dalili mbaya ya kujiua wenyewe.

 

Naibu Waziri Gekul akizungumza kwenye mbio za riadha za  Manyara Tanzanite Marathon zilizofanyika leo Desemba 17, 2022 Viwanja vya Kwaraa Mjini Babati, amesema magonjwa yasiyo ambukiza kama vile Presha na Sukari yanawaangamiza wengi kutokana na kutokufanya mazoezi.

 

Amesema kwa maisha ya sasa kulingana na aina ya vyakula vinavyoliwa na vyombo vya usafiri kuwepo kwa wingi watu hawana muda wa kutembea mwendo mrefu tofauti na miaka ya nyuma nchi ilipotoka.

 

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hasan anawajali wananchi wake ndo maana alitangaza kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi iwe siku ya mazoezi kwa watu wote.

 

“Vile ambavyo unakula, vile ambavyo unakunywa hakikisha unafanya mazoezi, usipofanya mazoezi ndugu yangu umekwenda kwa maisha sasa kwa maana zamani tunatembea kilomita zaidi ya 20 kwenda na kurudi shule, siku hizi watoto wanabebwa kwa mabasi, anapelekwa, anarudishwa, tunaua watoto wetu”

 

Amewataka walimu katika shule zote nchini kuhimiza michezo kwa watoto kwa vitendo ili kulinda afya zao.

 

Mbio zilizokimbiwa katika  Manyara Tanzanite Marathon ni  KM 42, 21, 10, na Mita 100, 400 Pamoja na 1,500 kwa wanaume na wanawake kutoka maeneo mablimbali ya nchi ya Tanzania.

 

Viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa ( BMT), Neema Msitha, baadhi ya  Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Manyara, Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, pamoja na Wananchi wa Babati  wameshiriki.

 

Washindi katika mbio hizo wamekabidhiwa zawadi zao uwanjani hapo yalipofanyika mashindano hayo  ikiwemo pesa taslimu pamoja na medali.

Share To:

Post A Comment: