Licha ya kuwepo kwa changamoto kubwa ya barabara na usafiri,  Bohari ya Dawa (MSD) imekuwa sio kikwazo kufikisha dawa na vifaa tiba katika Zahanati  ya Baga iliyopo Wilaya ya Morogoro Vijijini ambayo ipo kwenye miinuko mikubwa ya Milima ya Uruguru. Pichani wananchi wakisaidia kuzifikissha dawa katika Zahanati hiyo huku wakivuka mto.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Licha ya changamoto ya miundombinu ya usafirishaji katika baadhi ya maeneo, Bohari ya Dawa (MSD) imesisitiza itaendelea kupeleka dawa na vifaa tiba kila kona ya nchi ilikutoa huduma kwa wananchi..

Changamoto ya miundombinu ya usafirishaji katika baadhi ya maeneo, inailazimu Bohari ya Dawa (MSD) kutumia gharama za ziada kufikisha huduma kwa wananchi.

Zahanati ya Baga iliyopo Mnewele mkoani Morogoro ni kielelezo cha maeneo yaliyogubikwa na changamoto hizo.

Kulingana na jiografia ya eneo hilo, ni vigumu kutumia usafiri wa gari, hivyo wanalazimika kutumia gharama za ziada kukodisha pikipiki na baadaye watu kwa ajili ya kubeba ili kufikisha dawa na vifaa tiba katika zahanati hiyo.

Akizungumza Desemba 8, 2022 katika ziara ya maofisa wa MSD mkoani Morogoro, Dereva wa MSD, Kanda ya Dar es Salaam, Said Tindwa alisema kwa hali ilivyo ni vigumu kufika na gari.

"Gari unaenda nayo kama kilometa tatu kutokea barabara kuu, unafika eneo linaitwa Mtombozi hapo ndipo gari inaishia, hadi kufika ilipo zahanati ni safari ya takriban kilometa 60," alisema.

Katika safari hiyo, alieleza baadhi ya maeneo yanapitika kwa bodaboda na mengine wanalazimika kukodi watu wabebe mzigo kichwani hadi ilipo Zahanati ya Baga.

"Safari ya pikipiki ni kama nusu saa inakufikisha mtoni hapo pikipiki haiwezi kwenda tena tunawalipa watu wabebe mzigo kwa kichwa safari ya masaa mawili hadi wanafika," alieleza.

Mfamasia wa MSD katika Kanda hiyo, Diana Kimario amesema pamoja na ugumu wa mazingira, lakini hakuna zahanati itakosa kufikishiwa huduma.

"Ni kweli baadhi ya maeneo ni magumu kufikika lakini kama MSD tunawahakikishia wananchi kwamba tutawafikishia dawa na vifaa tiba huko huko walipo," alisema.

Vijana waendesha bodaboda wakipakia maboksi ya dawa kwenye pikipiki zao tayari kwa safari ya kuzipeleka Zahanati ya Baga ambayo ipo eneo lenye changamoto ya kufikiwa kiurahisi kutokana na kuwa na changamoto ya miundombinu ya barabara.

Dawa na vifaa tiba zikishushwa kwenye gari tayari kupelekwa Zahanati ya Baga. 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: