WAZIRI wa maji, Jumaa Aweso amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga kuipa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Dawasa), Sh milioni 500, ili mamlaka hiyo ikamilishe kazi ya kuunganisha maji kwa wananchi wa Jimbo la Kawe wanaohudumiwa na mradi wa maji wa Mapinga Bagamoyo, Mbweni na Tegeta A.

Aweso ametoa maagizo hayo leo Desemba 21, 2022 alipowasha pampu ya maji ya Mapinga hadi Changanyikeni yenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,225 uliogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 70

“Namuagiza Katibu Mkuu alete Sh milioni 500 hapa kwa sababu waliopo ndani ya scope wakipata maji na wengine wakakosa tutatengeneza chuki,” amesema.

Amesema, uwekezaji  uliofanyika ni mkubwa na kwamba dhamira ya Rais Dk  Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watu wote wanapata maji.

Pia Aweso ameitaka Dawasa  kuwaunganishia wateja maji ndani ya siku saba tangu wanapotuma maombi.

“Mteja anapoomba kuunganishiwa maji maji ndani ya siku saba awe ameshapata maji, sio danadana nyingi, na nitalifuatilia hili,” amesema.

Awali Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Cyprian Luhemeja alisema mtandao wa mabomba  Kilomita 1,226 wa mradi wa maji Bagamoyo mpaka Changanyikeni umekamilika pia umehusisha matenki matatu ya  Vikawe, Mbweni na Tegeta A.

Pia Busta mbili ambazo zina pampu sita, maeneo yote korofi yamekamilika, kilichobaki ni kufanya maunganisho kwa wananchi.

“Wananchi wa Bagamoyo, Kerege, Mapinga, Mbweni, Mivumoni, Madale, Changanyikeni, Goba, Mabwepande sasa  changamoto ya maji imekwisha,” amesema Luhemeja.

Naye Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima aliishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwezesha mradi mkubwa wa maji katika jimbo lake na kuondoa changamoto ya maji kwa wananchi wake.

“Sasa naweza kutembea kifua mbele kuwaeleza wananchi wa Jimbo la Kawe kero ya maji sasa imefika mwisho, tulikua tunakunywa mchuzi, sasa nyama chini tumeshazikuta,” amesema Gwajima.

Share To:

Post A Comment: