Na John Walter-Manyara

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Manyara imemuhukumu  Shamswadini John (35) mkazi wa Hanang Mkoani Manyara Maarufu kama Sikukuu  Kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kuua kwa kukusudia ambapo amemuua  mke wake aitwae Asia John (25) na mtoto wake Ahmedi Shamswadini (09).

Hukumu hiyo imetolewa  Desemba 7,2022 na Jaji Devotha Kamzola  ambapo amesema Mshtakiwa Shamswadini alimuua mke wake kwa kumnyonga,ambapo wakati akitekeleleza mauaji hayo mtoto alikuwa akipiga kelele hivyo baada ya kumuua Mama akarudi kumuua na mtoto, baada ya kufanya hivyo alichimba shimo kuufukia mwili wa mke wake lakini alipotaka kuufukia mwili wa mtoto alishindwa kufanya hivyo kwa kuhofia kuwa kumeshaanza kukucha na watu watamuona hivyo akaamua kwenda kuutupa mwili wa mtoto katika bwawa ili kupoteza ushahidi.

Uchunguzi wa daktari umeonyesha ni kweli wamefariki kwa kukosa hewa baada ya kunyongwa huku Wakili wa Serikali Petro Ngassa akiiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.

Muuaji alifanya tukio hilo limetokea 31/10/2018 huko katika Kijiji cha Hideti Hanang huku chanzo cha mauaji hayo ikiwa ni Ugomvi uliotokea mara baada ya mwanaume kuongeza mke wa pili jambo lililomchukiza mke wa kwanza  na kuamua kuhama nyumba ambapo aliamua kwenda kupanga chumba na kuanza kuishi na mtoto wake huko.

Jaji  Kamzola alisema baada ya mwanamke huyo kuhama (Asia) ndio Mwanaume aliposhikwa na hasira na kuhisi mwanamke huyo kuwa na mahusiano mengine na kupelekea kutekeleza mauaji hayo.

Awali mshtakiwa alikana kuhusika na mauaji hayo lakini baadae alikiri nakwenda kuonyesha sehemu aliyofukia mwili huo wa mke wake na baada ya kufukuliwa ulikutwa ukiwa na kanga shingoni.

 

Share To:

Post A Comment: