Na  Magesa  Magesa,Arusha


KAMPUNI  ya simu ya Vodacom Kanda ya Kaskazini inatarajia kugawa simu
milioni 1.5 kwa vikundi vya polisi shirikishi lengo likiwa ni kusaidia
kurahisisha mawasiliano kati ya vikundi hivyo na jamii.

Meneja wa Vodacom,kanda ya Kaskazini George Venanty aliayasema hayo
jana alipokuwa akigawa simu  kwa baadhi ya vikundi hivyo katika mitaa
33  jijini hapa na kusema kuwa zoezi hilo litakuwa likifanywa kwa
awamu lengo likiwa ni kuvifikia vikundi vyote katika kanda ya
kaskazini.

“Sisi Vodacom tunaamini katika amani utulivu na usalama wa jamii na
ndio maana tumeamua kutoa simu hizo ili kurahisisha mawasiliano  pindi
jamii inapoona kunataka kutokea tukio la uhalifu kuweza kuwasiliana
moja kwa moja kupitia simu hizo ambazo zina namba maalumu”alisema
Venanty.

Aliongeza kuwa waliamua kutoa simu hizo sio tu kwa kurahisisha
mawasiliano bali bia ni kurudisha sehemu ya faida wanayoipata  katika
kusaidia jamii na kuwataka wale wote watakaokabidhiwa simu hizo
kuhakikisha kuwa wanazitunza na kuzitumia kwa lengo lililokusudiwa.

Alisema kuwa simu hizo zitakuwa na namba maalumu ambazo zitakuwa
zikiratibiwa na jeshi la polisi ambapo endapo mwananchi atahisi
kunataka kutokea au kumetokea tukio la uvunjifu wa amani atatakiwa
kuwasiliana moja kwa moja kupitia simu hizo.

Kwa upande wake kaimu Kamanda wa polisi Mkoani hapa,Mary Kipesha
aliipongeza Vodacom kwa msaada wao huo na kusema kuwa umekuja wakati
muafaka kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na
uhalifu mkoani hapa.

Aliongeza kuwa usalama wa raia na mali zake ndio kila kitu na ndio
maana jeshi la polisi liliamua kuweka wakaguzi wa polisi kila Kata ili
washirikiane na vikundi hivyo vya polisi shirikishi katika kupamabana
na kukabiliana na uhalifu.

“Sisi polisi  lengo letu ni kuhakikisha tuna pata taarifa za uhalifu
kabla uhalifu huo haujatokea  ili tuweze kuwabaini wahalifu na
kukabiliana nao mara moja na ndio maana tuliamua kuunda vikundi hivi
na tayari vimeonyesha kuleta tija katika jamii inayowazunguka”alisema
Kipesha.

Naye Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha  Edith Swebe aliitaka jamii
kuhacha mara moja kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwani  jeshi la
polisi halitasita kumchukulia hatua kali yeyote Yule atakayebainika
kujihusisha na vitendo hivyo.

Alisema kuwa jukumu la kulinda usalama sio la jeshi la polisi pekee
bali ni la kila mtu hivyo wakati umefika kwa kila mwananchi kuwa
mlinzi wa mwenzake kwani lengo likiwa ni kukabiliana na uhalifu kwani
Arusha bila uhalifu inawezekana
Share To:

Post A Comment: