Na Dotto Mwaibale, Chalinze, Pwani
JUMLA ya Kaya nne katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani zimepata matokeo
chanya baada ya kuwezeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kupewa Sh.Milioni 2 kwa ajili ya
ufugaji wa kuku na kufanya biashara ndogondogo.
Wanufaika wa mfuko huo watatu kutoka Kitongoji cha Chahua na mmoja wa Kijiji cha Saleni
wakizungumza kwa nyakati tofauti leo Novemba 2, 2022 walielekeza shukurani zao kwa Rais Samia
Suluhu Hassan na TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kwa msaada huo
mkubwa uliobadilisha maisha yao.
Mnufaika Said Kiwamba wa Kitongoji cha Chahua ambaye anafuga kuku wa
kienyeji anasema anamatarajio makubwa baada ya kuwezeshwa Sh.250,000 kwa awamu
ya kwanza ambapo alinunua kuku 20 ambao wamekuwa vizuri na sasa wameanza kutaga
mayai.
"Nategemea kupiga hatua kubwa ya maendeleo kwani matunda ambayo
yametokana na fedha za awali Sh.250,000 nilizopewa na TASAF nimeyaona na siku
mbili zilizopita nimepewa tena Sh.250,000 jumla ni Sh.500,000 fedha hizi
zinanipeleka katika maendeleo mengine zaidi nashukuru sana TASAF" alisema
Kiwamba.
Kiwamba anasema kutokana na fedha alizozizalisha kwa ufugaji zinamsaidia kusomesha watoto na matarajio yake
ni kuendelea kufuga kuku wengi ili aweze kubadilisha maisha yake kwa kujenga
nyumba ya kisasa.
Mnufaika mwingine wa kitongoji hicho Zaina Rufubwa ambaye anafanya biashara
ya genge anasema sijui hali ya maisha na familia yake yangekuwaje bila
uwezeshaji huo wa TASAF kwani imewabadikisha mno kupitia fedha walizopewa kupitia Rais Samia Suluhu Hassan.
"Famailia yetu imekuwa na furaha sana na ari ya kukuza genge letu
lenye bidhaa mbalimbali ambalo linatoa huduma kwa jamii iliyopo katika
kitongoji hiki" alisema Rufubwa.
Rufubwa alisema matarajio yao ni kukuza mtaji waliopewa ili wawe na duka
badala ya genge kwa kuwa tayari tena wamepokea Sh.250,000 kutoka TASAF na kuwa
hivi sasa hata uhakika wa kupata chakula, mavazi na mahitaji mengine ni mkubwa
mno ukilinganisha na hapo awali.
Mnufaika wa TASAF wa kitongoji hicho Fatuma
Pononga alisema ndoto zake ni kuendeleza ufugaji hadi awe mfugaji mkubwa
na baada ya hapo ajenga nyumba kubwa ya kisasa na kununua gari litakalokuwa
likimrahisishia kazi katika shughuli yake ya ufugaji.
Bibi Mwajabu Mrisho mnufaika wa TASAF wa Kijiji cha Saleni ambaye
anajishughulisha na ufugaji wa mbuzi baada ya kupewa Sh. 216,000 awamu ya kwanza
ambapo alinunua mbuzi wanne anasema licha ya ufugaji huo kuwa na changamoto za
hapa na pale hawezi kuacha kwa sababu matunda yake ameyaona.
"Naishukuru sana TASAF na Rais Samia, mwanzo
nilikuwa na mbuzi niliokuwa nawafuga baada ya kuwezeshwa na wadau wengine nikiwa
na wenzangu kutokana na ujane wetu lakini TASAF ndio walikuja kuniongezea nguvu
kwa kunipa fedha hizo na kuongeza mbuzi wanne" alisema Bibi Yusuph.
Alisema matamanio yake ni kuona anakuwa mfugaji mkubwa wa mbuzi ndani ya kijiji hicho na nje na kuwa amekuwa akitembelewa na jamii ya wafugaji wa kimasai ambao wanampa mbinu mbalimbali akiwepo mwangalizi wake ambaye ni mratibu na mshauri wa masuala ya ufugaji kutoka Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Lugoba.
Post A Comment: