Na Denis Chambi, Tanga.

 Taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru kutoka mkoani Arusha imefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Shimuta kwenye mchezo wa mpira wa miguu baada ya kuichapa Taasisi ya Benjamini Mkapa bao 1-0 kwenye mchezo wao wasaka tiketi ya kupenya na kusonga mbele . 

Ukiachana ushindi huo wa 1-0 uliowavusha kiunzi cha makundi Tengeru wameendelea kuwa mwiba mkali kwa timu pinzani walizokutana nazo mpaka sasa kwani wamecheza michezo mitano bila kupoteza wakitoka sare moja tu hali ambayo inaonyesha kuwa wanajambo lao kwenye mashindano hayo mwaka huu. 

Akizungumza na waandishi wa habari mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Bakari George amewapongeza wachezaji wake kuingia kwenye hatua hiyo na kuonyesha jinsi walivyoyatapania mashindano hayo wakutamba kuwa wao pekee ndio wataing'arishana kuiwakilisha vyema kanda ya kaskazini kwa kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri mpaka fainali ili waweze kutwaa kombe kwenye soka na michezo mingine . 

"Kwetu hii ni faraja kubwa kuingia hatua ya 16 bora na hatujapoteza hata mchezo mmoja hii inaonyesha wazi namna taasisi yetu ilivyojipanga na kuwekeza kwenye timu yake ya watumishi mpango wetu sis ni kushinda michezo yote, tumecheza michezo hii kwa kanda ya kaskazini na tuliongoza, ninachowaambia ni kwamba sisi falsafa yetu ni mpira maendeleo na katika taasisi zote zilizotokea Arusha sisi ndo ambao tutarudi na kikombe na tutaing'arisha kanda ya kaskazini kwa ujumla" alisema Dkt. George 

Nahodha wa kikosi hicho Elifadhili Mpehongwa amesema haikuwa rahisi kwao kuingia katika hatua hiyo kutokana na ushindani waliokutana nao akitamba kuwa matokeo wanayoyapata sasa hivi yanasadifu maandalizi waliyoyafanya kwa mwaka mzima wakijifua kuelekea mashindano hayo hivyo kwao sio bahati mbaya kuzidi kufanya vizuri wakitangaza vita kwa timu watakayokutana nayo kwenye hatua ya 16 bora.

 "Sisi tuliwaambia watu kuwa tumekuja kuchukuwa kikombe tumefanya mazoezi mwaka mzima timu yetu mpaka kufika hapa ni nzuri kwa sababu imejiandaa tunawahakikishia kwamba hatua ya 16 bora tutafanya maajabu zaidi, ilikuwa ni ngumu sana kuvuka na kwenda hatua ya 16 bora kwa sababu kila timu ilijipanga lakini timu yetu ni ya mapambano na wachezaji wanajituma"alisema Mpehongwa. 

Kwa upande wake katibu wa michezo kutoka taasisi ya Benjamini Mkapa George Bwire amekiri ushindani uliopo kwa baadhi ya timu ambao kwa namna moja ama nyingie ndio umewakwamisha kushindwa kusonga mbele katika mshindano hayo wakiahidi kwenda kuanza masandalizi mapema kwa mwaka ujao ili wasiishie njiani tena. 

"Tunaamini kabisa kwamba mashindano haya ya Shimuta yamekuwa na upinzani mkubwa sana ,ni awamu ya pili tunashiriki mashindani haya ninaamini walimu na viongozi wameona jinsi timu zetu zilivyofanya tunakwenda kurekebisha na ninaamini mwakani tutakuwa vizuri zaidi" alisema Bwire 

Mashindano hayo yanayoshirikisha mashirika ya umma ,taasisi binafsi na makampuni yalianza kurindima November 15 kwa michezo mbalimbali kuchezwa kwenye viwanja tofauti tofauti jijini Tanga ambapo yanatarajia kuhitimishwa rasmi November 29, 2022.
Share To:

Post A Comment: