Picha/UN

Na Immauel Msumba; Longido 

Afya ya uzazi ni huduma inayotolewa kwa wanawake, wanaume na vijana walio katika umri wa kuzaa. Huduma hii inajumuisha magonjwa ya uzazi yanayohusisha ; kupanga uzazi, ujauzito, magonjwa ya kujamiiana, ukeketaji na mila potofu, saratani ya via vya uzazi, kuzuia na kutibu ugumba. Huduma ya afya ya uzazi imeendelea kuboreshwa nchi nzima kwa kiwango cha kuridhisha. 

Makundi mbalimbali yanashiriki katika kupata huduma hizi katika vituo vya kutolea huduma. Hata hivyo, kutokuwepo kwa elimu na uhamasishaji wa kutosha wa afya ya uzazi kwa makundi mbalimbali na hasa vijana na wanaume kumesababisha kuongezeka kwa magonjwa ya ngono pamoja na matatizo ya mimba zisizotarajiwa, hasa maeneo ya vijijini. huku mila potofu zikichangia katika kuzorotesha afya ya uzazi katika baadhi ya maeneo.

Katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha ambapo Wananchi wengi ni wa Jamii ya Kimaasai wamekuwa wakikosa huduma ya Afya ya uzazi kutoka na shughuli zao za kifugaji zinazofanywa na wananchi hao kutokana na kuishi maisha ya kuhamahama jambo ambalo linasababisha wananchi wa maeneo hayo kutofikiwa na wataalamu wa Afya kwa wakati. 

Wakina mama wengi Wilayani humo wanakosa elimu ya afya ya uzazi kutoka na muda mwingi kuutumia katika shughuli za kutafuta maji na kiufugaji kutokana na kuhamahama kwao hali inayosababisha kutofikiwa na wataalamu wa afya kutokana na mazingira wanayoishi.

Nemelock laizer ni Mama wa watoto sita na hapa anaeleza kuwa yeye kama mama wa kimasai wanahitaji sana elimu ya Uzazi kwani ndio kitu cha muhimu kwa wakati wa sasa ili kuweza waweze kuelimishwa juu ya Afya ya Uzazi  na umuhimu wa kujifungulia  kituo cha kutolea huduma .

"Jamii yetu ya kifugaji bado tuko nyuma sana kwa upande wa kuhamasika kujifungulia hospital kwanza wengi wetu tunaamini kujifungulia hospitali ni woga ndiyo inatupeleka huko  kwamba tunashindwa kuvumilia uchungu, lakini pia hii tabia tumejengewa na kizazi kilichopita kwamba mama lazima ajifungulie nyumbani na hadi upelekwe hospital ni dakika za mwisho sasa imeonekana hakuna njia nyingine kitu ambacho kinaweza kusababisha madhara kwa mama na mtoto pia" Ameleza Namelock

Namelock ameiomba Serikali kuongeza Wataalamu wa maswala ya kinamama katika vituo kwani changamoto kubwa wanayokutana nayo kwenye vituo katika maeneo yao wamekuwa si wataalamu sana hali ambayo huduma wanazopatiwa kuwa haziridhishi huku wakiomba kupatiwa semina mara kwa mara juu ya Afya ya Uzazi.

Kwa Upande wake Dokta Suleiman Mtendela Mganga Mkuu Halmashauri ya Longido amesema  swala la Uzazi , au watu kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma  jambo hilo ni muhimu kwa  kina mama kujifungulia vituo vya afya ili kuweza kuwa salama kwa afya zao.

Dkt. Mtendela ameongeza kuwa wakati wa kujifungua kuna mambo mengi yanayoweza kujitokeza, ikiwemo mtoto kuzaliwa salama  bila matatizo yeyote lakini baada ya kuzaliwa anahitaji kufanyiwa mambo mbalimbali  ambayo akiyakosa mtoto anaweza kupata shida au mama anayehusika.

"Lakini eneo la pili mama anaweza kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua ,lakini pia mtoto anaweza akawa anashindwa kupumua vizuri , kwa hiyo umuhimu wa kujifungua katika vituo vya kutolea afya ni kuweza kukabiliana na matatizo yanayoweza kujitokeza pale mama anapokuwa amejifungua , na ndio maana Serikali inachukua juhudi mbalimbali ili kuhakikisha wakina mama wajifungulia katika vituo vya kutolea huduma "Dkt. Mtendela.

Sambamba pia amesema kwa Halmashauri ya Longido wastani wa kina mama zaidi ya mia mbili (200) kila mwezi wanaojifungua lakini kwa asilimia 70 wengi wao wanajifungulia vituo vya Afya, "kwa Hali hii asilimia 30 Bado ni kubwa ka sababu tusipokuwa makini tunaweza kusababisha kupoteza vifo vilivyotokana na Uzazi ambapo asilimia 30 ya hawa kina mama wangeweza kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma tungeweza kuokoa maisha yao au matatizo ya kiafya yanayotokana na uzazi, kwa juhudi mbalimbali zinazofanya na Serikali kuongeza Watumishi Longido tumepokea watumishi zaidi ya 50 kwa kipindi hiki kifupi ,lakini pia Serikali imeongeza majengo na bado inaendelea kuongeza". Dkt. Mtendela.

Diwani wa Kata ya Mundarara Wilayani Longido Alais Mushao anaeleza kuwa kuhamahama kwa mifugo kwa ajili ya kutafuta nyanda za malisho ni chanzo cha Wanawake wa jamii ya kimaasai kukosa Elimu ya Afya ya Uzazi kutokana na Wataalamu kutowakuta kwenye maboma yao wakati wa utoaji wa Elimu kulingana na kuhamahama kwa mifugo yao .

"Changamoto ni kubwa sana Vituo vya Afya nivichache na kwa uchache huo bado viko mbali sana na maboma, lakini pia jamii yetu ya kifugaji inapitia wakati mgumu kwenye swala la Afya ya Uzazi , pia pamoja na hayo yote swala la barabara pia ni changamoto kubwa sana katika  kufikikia vituo hivyo  unakuta Kata ina Vijiji 4 zahanati ni 1 wataalamu hawatoshezi zahanati unakuta ina watoa huduma wawili {2}"ameeleza Dkt. Mushao 

Sisi kama Baraza la madiwani kwa kuendelea kushirikiana na Serikali tunaendelea kuongeza Vituo vya Afya pampoja na zahanati kwa kila Kata ikiwezekana kila Kijiji kiwe na zahanati , ili iwe rahisi zaidi mwananchi kufikiwa na huduma , lakini pia mbali na waajiriwa wataalamu wa kutoa semina kwa lengo la kuhamasisha jamii ya kifugaji jambo ambalo baadhi yao hawana uelewa juu ya Afya ya Uzazi na maswala ya Afya kwa ujumla


Share To:

Post A Comment: