Mkurugenzi wa Uandaaji wa Viwango TBS, Bw.David Ndibalema akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Kilele Cha Maadhimisho Siku ya Viwango Duniani Kwa mwaka 2022 nchini Tanzania.


**********************


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM


KATIKA kusheherekea Siku ya Viwango Duniani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa wiki mbili kwa ajili ya kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya viwango ikiwemo , faida zilizopo na umuhimu wa wadau kushiriki katika utayarishaji na uandaaji wa viwango .


Ameyasema hayo leo Novemba 2, 2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uandaaji wa Viwango TBS, Bw.David Ndibalema wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuelekea Kilele Cha Maadhimisho Siku ya Viwango Duniani Kwa mwaka 2022 nchini Tanzania.


Amesema wiki ya kwanza wataitumia vyombo vya Habari kwa kuelimisha jamii kuhusu masula ya viwango ikiwemo uandaaji wa viwango hivyo. Wiki inayofuata tarehe 14 Novemba 2022 kutakuwa na mkutano wa wadau mkoani Morogoro ambao unalenga kujadiliana kuhusu dhima au kauli mbiu ya mwaka huu "VIWANGO KWA MAENDELEO ENDELEVU ( SDGs)" na kuelezea namna wanavyoweza kushiriki kwenye mchakato wa uandaji wa Viwango na kuangalia mchango wa Viwango katika SDG na maisha ya kila siku ya Mtanzania.


"Tarehe 18 Novemba 2022 tutakuwa na mkutano wa wadau hapa Dar es Salaam, ambapo pia utahusu mjadala mpana na kutafakari kuhusu kauli mbiu ya mwaka huu lakini pia tutatumia fursa hiyo kuzindua rasmi mashindano ya insha Kwa mwaka 2022/2023 yenye lengo kubwa la umuhimu wa viwango katika shughuli mbalimbali za kiuchumi. Mashindano haya hufanyika kila mwaka na hushindanisha wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini". Amesema


Aidha amewashukuru wataalamu mbalimbali na wadau ambao wamekuwa wakishiriki katika kuandaa viwango ambavyo vinaratibiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS)


Pamoja na hayo ametoa wito kwa wadau wakiwemo wazalishaji wa bidhaa mbalimbali na wajasiriamali kuendelea kushiriki kwenye uandaaji viwango lakini pia kutumia viwango ambavyo vinaandaliwa ili tuweze kufikia malengo ya kuwa na ulimwengu uliobora kwa kuwa na maendeleo endelevu.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: