Nahodha wa timu ya mpira wa miguu kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanayama pori Tanzania 'TAWA' Ernest Carlos akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya timu yao kutolewa kwenye mashindano ya SHIMUTA hatua ya robo fainali na shirika la viwango Tanzania TBS kwa mikwaju ya penati 4-5.
Kocha wa timu ya mpira wa miguu ya Mamlaka ya usimamizi wa wanayama pori Tanzania 'TAWA' Abdallah Msauka akizungumza mara baada ya mchezo wao wa robo fainali ya mashindano ya SHIMITA waliocheza dhidi ya timu ya shirika la viwango Tanzania 'TBS'..
Na Denis Chambi, Tanga.
TIMU ya mpira wa miguu kutoka Mamlaka ya usimamizi wa wanayama pori Tanzania 'TAWA' imetupwa nje ya mashindano ya Shimuta kwa njia ya mkwaju ya penati 4-5 kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali walipokutana kutafuta tiketi ya kuwania nafasi ya nusu fainali na wapinzani wao Shirika la viwango Tanzania 'TBS' katika mchezo uliochezwa kwenye dimba la Popatlal jijini Tanga.
Licha
ya kuyaaga mashindano hayo lakini bado timu hiyo inajipongeza kwa hatua
ya kuvuka malengo walilokuwa wamejiwekea ambapo walizamilia kuvuka
hatua ya 16 bora ambayo walifanikiwa na hatimaye kuja kugonga mwamba
kwenye robo fainali huku wakiwa na rekodi nzuri kwenye michezo
waliyocheza ambapo hawajapoteza hata mechi moja.
Katika
mchezo huo ulioamuliwa na mikwaju ya penati zilimalizika dakika zote
ndani ya uwanja kwa droo ya 1-1 TAWA wakitangulia kupata bao la mapema
kabisa kunako dakika ya tatu kwenye kipindi cha kwanza ambapo
haikuchukuwa muda TBS nao wakasawazisha kunako dakika ya 16.
Nahodha
wa timu hiyo Ernest Carlos alisema malengo ya mamlaka ya usimamizi wa
wanayamapori Tanzania TAWA ilikuwa ni kuvuka hatua ya 16 bora ambayo
walifanikiwa kuitimiza na kufanikiwa kupiga hatua moja mbele kitu
ambacho wanajivunia licha ya kuwa walitamani kucheza fainali za
mashindano hayo kwa mwaka huu wa 2022.
"Malengo
ya mamlaka ya usimamizi wa Wanayama pori 'TAWA' ilikuwa ni kuvuka hatua
ya 16 bora, tumefanikiwa lengo limetimia tumecheza robo fainali
ilikuwa ni zaidi ya lengo tulilokusudia" alisema Carlos.
Alisema
mbali na kushiriki michuano hiyo walikuja na ujumbe maalumu kwa
wananchi na Tanzania kwa ujumla wa kutunza mazingira na wanyama wote
ambao wapo nje ya hifadhi za taifa ambapo amewataka kushirikiana na
mamlaka hiyo katika kuhakikisha wanalinda na kutunza hifadhi zote
zilizopo hapa nchini.
"Lakini
pia lengo la taasisi lilikuwa ni kuleta motisha kwa wafanyakazi pamoja
na kuitangaza mamlaka ya usimamizi wa wanayamapori kuwajulisha wananchi
kuwa kuna mamlaka kama hiyo ambayo inahusika na wanyama pori wote ambao
wako nje ya hifadhi za taifa zote, kikubwa tushirikiane wote kulinda
mazingira yetu kutunza wanyama wetu ili tuweze kuwarithisha vizazi
vijavyo" alisema Carlos.
Akitoa
tathmini ya mchezo huo kocha anayekiongoza kikosi cha timu ya TAWA
Abdallah Msauka amesema kuwa siku zote hatua ya kuamua mchezo kwa njia
ya penati haina mwenyewe licha ya kuwa waliweza kutawala mchezo huo kwa
dakika zote, huku akijivunia ubora wa timu yake ambayo ni mara ya pili
kushiriki michuano hiyo.
"Mchezo
ulikuwa ni mzuri tulifanikiwa kupata goli dakika ya tatu wenzetu
wakaja kusawazisha dakika ya 16, kipindi cha pili pia tumecheza kila
mmoja alikuwa anatafuta nafasi ya kupata goli lakini hatukufanikiwa
tumekwenda kwenye penati wenzetu wametuzidi penati moja kwahiyo ndio
sehemu ya mchezo hapa tulipofikia kwa hatua hii kwenye mashindano yajayo
tuna kitu cha kuanzia"
"Ndani
ya mchezo sijazidiwa ila penati ndio ziliamua na ilikuwa lazima mmoja
akose ili mwingine apite lakini kikubwa namshukuru Mungu kwasababu timu
ilikuja kwenye mashindano ikiwa ni mara ya pili kushiriki lakini kuna
timu ambazo ni uzoefu zimeondoka kabla yetu kwahiyo kwa mimi mwalimu
kuwa na timu ya TAWA kwa mara ya kwanza naona kabisa ni hatua
nimepiga" alisema Msauka.
Mashindano
hayo yaliyoanza kutimua vumbi November 15 yanahusisha timu za
watumishi kutoka mashirika ya umma, taasisi binafsi na makampuni kote
nchini na yanatarajiwa kutamatika November 29 mwaka huu kwa fainali za
michezo ya mpira wa miguu, Kikapu, Wavu, Pete , pamoja na michezo
ya jadi ikiwemo Draft, Dats riadha yakibebwa na kauli mbiu isemayo
'Shimuta familiya moja' .
Post A Comment: