Naibu Waziri wa Kilimo,  Anthony Mavunde abainisha mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji mbegu bora zenye virutubisho vya kibaiolojia ili kuimarisha lishe na kupunguza udumavu kwa wananchi hususan wanawake na watoto.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 17 Novemba, 2022 alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wenye lengo la kuimarisha na kuongeza uzalishaji wa mazao yenye virutubisho vya kibaiolojia uliofanyika Jijini Dar es Salaam chini ya uratibu wa Shirika la AGRA nchini. 

"Utapiamlo ni changamoto kubwa ambayo nchi yetu tunaendelea kukabiliana nayo. Serikali chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu tunatekeleza Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe “National Multasectoral Nutrition Action Plan” (NMNAP) 2021/22 - 2025/26 ambao una lengo la kukabiliana na utapiamlo katika aina zake zote.

Ni dhahiri kwamba Serikali imejidhatiti kuhakikisha kuwa changamoto hii inapungua kwa kasi ili kuondokana na madhara yatokanayo na utapiamlo ikiwemo udumavu na uzito chini ya kiwango.

Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huo wa NMNAP, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) iligundua mbegu bora ya maharage aina ya Jesca iliyoongezwa madini ya chuma na zinki na inafanya vizuri sokoni, na kuwataka wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na Serikali katika jitihada za kuzalisha mazao zaidi yenye mchango mkubwa katika lishe.

Suala la lishe ni kipaumbele kwa Serikali, na kupitia mradi wa Feed the Future, unaanzishwa mpango wa kutoa chakula chenye lishe bora mashuleni ili kuwezesha kukabiliana na changamoto ya utapiamlo nchini”Alisema Mavunde

Mkutano huo ulijumuisha wadau mbalimbali wakiwemo Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika la Mpango wa Dunia wa Chakula (WFP), Taasisi ya Rockfeller Foundation, Shirika la AGRA, Taasisi za Utafiti za Kimagaifa, Taasisi na Idara za Serikali, Wazalishaji wa Mbegu na Wakulima.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Shirika la Rockefeller Foundation katika Ukanda wa Mashariki, Bi. Betty Kitaara alieleza kuwa kwa kushirikiana na AGRA, wataendelea kushirikiana na Serikali kwenye mpango mbalimbali ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa lishe hususan kwa wanawake na watoto.

Share To:

Post A Comment: