Angela Msimbira TABORA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinaimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ili kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati.

Ametoa agizo hilo leo Novemba 19, 2022 wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya elimu inayotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, mkoani Tabora.

Amesema kuwa Serikali kuu haiwezi kumaliza kila changamoto hivyo waweke mikakati ya kuzuia mianya ya upotevu wa mapato ili fedha hizo zitumika kwenye miradi ya elimu, Afya na miundombinu ya barabara.

"Tujitahidi katika kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato pasitokee uvujaji wa mapato, msiweke mawakala wa kukusanya mapato ambao watajinufaisha wenyewe na pasitokee watumishi kukusanya fedha na kujinufaisha wenyewe na kusiwe na matumizi ambayo ni kinyume cha utaratibu,"amesisitiza Waziri Kairuki.

Amezitaka Halmashauri hizo kuangalia thamani halisi ya fedha katika matumizi na manunuzi ya umma ziwe zinaakisi thamani ya fedha zilizotolewa kwa kuhakikisha taratibu za manunuzi zinafuatwa.

Waziri Kairuki pia amezitaka Halmashauri hizo kuhakikisha wanasimamia matumizi ya fedha na kuwa macho kwenye makadirio ya makusanyo.

Amewataka wakadiriaji majengo kuhakikisha wanafanya kazi ya kwa weledi na uaminifu katika kukadiria matumizi ya fedha za ujenzi wa majengo ya serikali huku akiwatak wakurugenzi kujiridhisha na makadirio yanayotolewa na wataalam.

Amewahimiza Wakurugenzi kuhakikisha kamati zinazosimamia ujenzi zinaelewa majukumu yao ipasavyo kwa kujua miongozo na taratibu zilizopo.

Aidha, amewataka viongozi katika ngazi za Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.



Share To:

Post A Comment: