Wakulima wa maeneo ya Chikuyu,Maweni na Kintinku wilayani Manyoni,Singida wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan na serikali ya awamu ya sita kupitia wizara ya kilimo kwa mikakati ya ujenzi wa miradi mipya ya umwagiliaji na ukarabati wa miradi ya zamani katika wilaya ya Manyoni.

Hayo yamesemwa leo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa .Anthony Mavunde katika miradi ya umwagiliaji za Chikuyu,Ntambaliza,Ngaiti na Udimaa ambapo amepata nafasi ya kukagua skimu hizo pamoja na kuongea na wakulima kuwakikishia azma ya serikali kuona skimu zote hizo zinafanya kazi ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kukuza uchumi wa wakulima.

“Mh Rais Samia anayo dhamira kubwa ya kumuona mkulima wa Tanzania ananufaika na kilimo chake kwa kulima kwa tija na kuongeza kipato kupitia kilimo cha uhakika cha umwagiliaji.

Mh Rais ameelekeza eneo la Mbwasa,Manyoni kujengwa bwawa lenye thamani ya Tsh 20bn lenye uwezo wa uhifadhi maji wa mita za ujazo milioni kumi pamoja na skimu za umwagiliaji katika eneo hilo.

Na mimi namuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kusimamia ukarabati wa kingo za mto za mradi wa umwagiliaji Chikuyu sambamba na kufanya usanifu wa miradi ya Ntambaliza,Udimaa na Ngaiti ili kuwa na chanzo cha uhakika cha maji na miundombinu ya mifereji ya maji ya umwagiliaji”Alisema Mavunde

Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo yaliyojitokeza,Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Ndugu Raymond Mndolwa amesema kwamba Tume imejipanga kuhakikisha miradi yote mipya ya skimu za umwagiliaji inakuwa na chanzo cha uhakika cha maji ili kuruhusu shughuli za kilimo cha umwagiliaji kufanyika zaidi ya mara moja kwa mwaka.

Naye Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Dr. Pius Chaya kwa niaba ya wakulima wote amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kupitia wizara ya kilimo kwa kazi kubwa ya miradi ya umwagiliaji inayofanyika katika Wilaya ya Manyoni ambapo kupitia miradi hiyo wananchi wa maeneo hayo watakuza vipato vyao na kutatua changamoto kubwa ya Ajira hususani kwa vijana.

 Mkuu wa Wilaya ya Iramba ambaye anakaimu wilaya ya Manyoni kwa sasa Suleiman Mwenda ameahidi kwa niabaya serikali ya wilaya kusimamia utekelezaji wa miradi hii kwa uadilifu na umakini mkubwa ili ilete matokeo chanya kwa wakulima wa mpunga wa skimu hizo.



Share To:

Post A Comment: