Na Asteria Muhozya, Arusha

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka Wajiolojia nchini kuhakikisha wanaiheshimisha taaluma yao kwa kutoruhusu wasio waaminifu  kuingilia majukumu ya kitaaluma kutokana na umuhimu wa shughuli za utafiti kwa maendeleo ya Sekta ya Madini  na Taifa.

Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (TGS) kwa mwaka 2022 unaofanyika jijini Arusha  na kuwashirikisha wajiolojia  wenye ubobezi wa aina mbalimbali  takribani 200 kutoka wizara, taasisi na kampuni mbalimbali nchini.

Amesema jiolojia ni sayansi muhimu kutokana na ukweli kwamba ili nchi iweze kuendelea kiuchumi inahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la jiosanyasi na kwa kuzingatia  Tanzania  ni nchi iliyobarikiwa kuwa na rasilimali za kutosha za madini hivyo, uwepo wa wanataaluma wabobezi kutaliwezesha taifa kukuza sekta ya viwanda kupitia sekta ya Madini.

Amesema kuwepo wa wajiolojia wadanganyifu kumepelekea wawekezaji wengi kupoteza fedha zao kutokana na kupatiwa taarifa zisizo sahihi hali ambayo imepelekea wawekezaji kupoteza imani ya kuwekeza kwenye sekta ya madini huku hali hiyo ikisababishwa na wajiolojia hao.


‘’ Wajiolojia ni moyo wa sekta ya Madini, hatuwezi kuchimba bila wao na badala yake tutachimba kwa kubahatisha. Kama taifa tunataka mambo yatokee kwa nguvu ya sayansi. Wajiolojia ndiyo wanaoleta fedha  za uwekezaji nchini,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.

Akizungumzia Bodi ya Wajiolojia, amesema kwamba Wizara iko katika hatua za mwisho  za kukamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa  bodi hiyo na kuongeza kwamba, baada ya Serikali kukamilisha  sehemu yake itatoa nafasi kwa  wadau hao kutoa maoni kuhusu namna gani bodi hiyo iundwe, namna itakavyosimamiwa,  masuala ya yatakayohusisha vyanzo vya fedha na kuangalia masuala ya sheria.


Ameongeza kuwa, wakati Serikali inakamalimisha mchakato wa kuundwa kwa  bodi hiyo  ni muhimu wajiolojia wakahakikisha wanaiendeleza taaluma ya jiolojia ili kuipatia nchi heshima ikiwemo  kuwawezesha wawezekaji kupata taarifa sahihi na hivyo kuvutia uwekezaji zaidi kwenye sekta ya Madini.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wajiolojia Elisante Mshiu amemweleza Waziri Biteko kuhusu kuwepo kwa changamoto kadhaa  katika kutekeleza shughuli za wanajiosayansi nchini  ambazo kwa kiasi flani zinachangia kuifanya taaluma kutoendelea.


Amezitaja changamoto hizo kuwa ni  pamoja na kuwepo kwa changamoto ya kukuza viwango  au uwezo wa kufanya tafiti kwa wahitimu wapya na kupendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kuweka wahitimu wapya kwenye kipindi cha mpito wakiwa wanafanyakazi  chini ya uangalizi au maelekezo ya wabobezi na wanaopata ujuzi stahiki wa vitendo wathibitishwe na kuruhusiwa kufanya tafiti wenyewe.

‘’Mheshimiwa mgeni rasmi, mfumo huu hutumika kwenye nchi nyingina pia kwenye taaluma mbalimbali nchini kama vile wahandisi, madaktari, wahasibu na kadhalika.

Mshiu amezitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na matokeo ya tafiti mbalimbali kuwa ya udanganyifu na chini ya viwango. Amesema kuwa, kwa bahati mbaya mara nyingi kuna watafiti ambao kwa makusudi wanatoa matokeo ya tafiti  yasiyo sahihi  na mara nyingi suala hilo hufanyika kwa makusudi. Akitoa mapendekezo ya changamoto hiyo,  Mshiu  amesema Chama Cha Wajiosayansi kinapendekeza kuanzishwa kwa mfumo wa uhakiki wa taarifa zinazotolewa na wataalamu hususan za miradi ya uzalishaji ili kuhakikiwa kuwa zinakuwa sahihi.


‘’   Hii itafanyika kwa kuwa na Bodi ya Uhakiki wa Taarifa, na kuwa mfumo wa kuthibitisha ubora wa taarifa hizo ambapo mtafiti akibainika ametoa taarifa zenye ubora wa chini ya viwango, hupewa adhabu stahili na mwingine kunyanga’nywa usajili hadi hapo atakaooonekana amejirekebisha,’’ amesisitiza  Mshiu.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewataka wajiolojia nchini kuwa waadilifu na kuweka nidhamu ya juu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao na kuongeza kwamba, sekta ya uziduaji inahitaji watu waadilifu.

‘’ Wizara imepewa jukumu la kusimamia sekta ya uziduaji na inahitaji uadilifu na nidhamu ya juu, sisi kama wizara tuko tayari kushirikiana kikamilifu nanyi na inatambua nafasi na kazi zinazofanywa na wajiolojia.

Naye, Rais wa Jumuiya ya Wajilojia Tanzania, Prof. Abdulkarim Mruma ameieleza hadhira hiyo kuhusu utajiri wa kijiolojia ambao nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa nao na kuelelezea namna bora ya kuitumia taaluma hiyo kwa maendeleo ya nchi na jamii nzima.

Sambamba na mkutano huo, zimetolewa tuzo kwa kampuni mbalimbali zilizochangia  kufanyika kwa mkutano huo  ikiwemo Mgodi wa Uchimbaji Dhahabu wa Geita, Shirika la Madini la Taifa  (STAMICO)  Kampuni ya BarrickGold, Vilevile mkutano huo umetumika kutoa tuzo  kwa wajiolojia wastaafu.

Awali, kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, wataalamu hao walitembelea katika vivutio vya utalii kujionea na kujifunza utalii wa kijiolojia katika maeneo ya Serengeti, Ngorongoro na Olduvai Gorge
Share To:

Post A Comment: