DENIS CHAMBI , TANGA.




Serikali imeziagiza Mamalaka za ajira kote nchini kuhakikisha kuwa zinaendelea  kutekeleza haki na stahiki zote za Watumishi wa Umma  ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti ya kila mwaka  ya  mafunzo pamoja na  mafungu ya Posho za watumishi ili kuwaweza kushiriki michezo ikiwa no haki yao kisheria.


Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Jenista Mhagama wakati akifungua rasmi mashindano yanayohusisha Watumishi wa Umma  kutoka wizara idara na taasisi zote za serikali Tanzania bara 'SHIMIWI' yanayoendelea mkoani Tanga ambapo amesema wizara inaendelea kusimamia maagizo ya serikali ya kuhakikisha kuwa Watumishi wote wenye sifa za kupandishwa madaraja yanatekelezwa.


"Niwaagize waajiri kote nchini kuhakikisha  Mamalaka za ajira katika utumishi wa Umma  wahakikishe wanatenga bajeti ya kutosha kila mwaka katika mafungu yao , kulipa stahiki za kisheria ikiwemo likizo mafunzo na posho ikiwemo posho ya kuhudhuria michezo katika nyanja ya kitaifa posho hizo zitengwe kwa sababu ni haki ya Watumishi wa Umma kushiriki michezo"


"Waajiri wote wahakikishe wanafuatilia kwa karibu mienendo ya Watumishi wa Umma nchini na utaratibu mzuri wa kuhakikisha kila mtumishi anapanda daraja bila kucheleweshwa na kuhakikisha upandishaji madaraja  hauna upendeleo wa aina yeyote" alisema Mhagama.


"Kwakuwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ametenga fedha za malimbikizo ya mishahara  niwaagize waajiri wote nchini kufanya uhakiki na kuleta taarifa  za Watumishi kwenye ofisi yangu ili Watumishi wote waweze kulipwa  malimbikizo yao kwa wakati, kuhakikisha waajiri  wanasimamia nidhamu kwa Watumishi ili waweze kuchangia maendeleo ya taifa." Aliongeza


Awali akizungumza mkuu wa mkoa wa Tanga Omari Mgumba  amewataka watumishi wote nchini kudumisha uzalendo uwajibikaji, maadili, nidhamu na kujitoa kwa maslahi mapana ya Taifa. 


"Nimpongeza Sana Raisi kwa kuendelea kuwekeza kwenye rasilimali watu  Kuna changamoto ya  Watumishi tuko wengi lakini maadili ya Utumishi wa Umma yanaendelea kuporomoka siku hadi siku  nidhamu , uzalendo kujitoa kwaajili ya taifa letu niwaombe sana Watumishi wote kuwa wazalendo kwa maslahi mapana ya Taifa letu" alisema Mgumba.


Kwa upande wake mwenyekiti wa shirikisho la SHIMIWI  Daniel Mwalusamba ameiomba serikali kuendelea kuzisimamia Mamalaka za michezo kupitia Watumishi wote wa Umma kuhakikisha kuwa ushiriki wa Watumishi unakuwa kwa wingi ili kuendelea kudumisha ushirikiano baina yao pamoja na kushiriki michezo kikamilifu


"Serikali iliweka utaratibu wa kuwashirikisha Watumishi wa Umma kupitia mashirikisho kwa niaba ya Watumishi naomba Mamalaka zinazohusika zisimamie kuhakikisha Watumishi wanashiriki kwenye michezo kwa kuzingatia taratibu zilizowekea na serikali sisi tutaendelea kuzingatia miongozo inayotolewa na vyombo vyote vinavyoaimamia michezo ikiwemo wizara yetu ya michezo" alisema Mwalusamba. 


Akizungumza katibu mkuu wa shirikisho la wafanyakazi wa serikali na afya Tanzania 'TUGHE' na  katibu mkuu wa shirikisho la wafanyakazi 'TUCTA' Henry Mkunda alisema kuwa  vyama hivyo vinaendelea kuwajengea uwezo Watumishi kote nchini  ilimara baada ya kustaafu waweze kujimudu katika maisha  yao na sii kutegemea stahiki zao pekee.


"Tunafurahi sana kwa sababu michezo hii ni afya , inayowashirikisha  wafanyakazi kutoka sehemu mbalimbali katika kujenga mahusiano  lakini,sisi  kama chama cha wafanyakazi hususani TUGHE wanaendesha mafunzo kwa wafanyakazi kuhusu kujiandaa kustaafu  kwamba wataishije wasitegemee mpaka wastaafu ndio wajifunze namna ya kuwekeza "


Awali akizungumza afisa masoko kutoka kampuni ya  Agricom Africa  ambao ni wadhamini wa 'SHIMIWI' kwa mwaka 2022 Baraka Konkara kwa kutambua umuhimu wa michezo  kwa kila mtu kuweza kupambana na magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza wanaungana na serikali katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii.


"Kampuni hiyo ilizindua kampeni ya  mtumishi shambani ambayo umejikita katika kuwainua wakulima kwa kuwawezesha huduma  mbalimbali pamoja na kumsaidia kupata matokeo chanya kupitia sekta ya Kilimo ambayo serikali imekuwa ikisistiza watanzania katika nyanja hiyo ili kuendelea kujikimu katika maisha"


"Tumeona kuwa serikali ya awamu ya sita imeweza  kutoa kipaumbele katika sekta ya  Kilimo hivyo sisi  kama wadau wa kilimo tumekuja na kampeni ya Mtumishi shambani ambapo tunatoa huduma pale mteja anaponunua vifaa kwetu , kumwezesha kupata mikopo kupitia sekta ya kifedha ili kuwasaidia wafanyakazi na Watumishi wa Umma wawze kufanya kilimo chenye tija"


Mashindano hayo  ya SHIMIWI ambayo yanahusisha michezo ikiwemo ya mpira wa miguu, kuvuta kamba , mbio za baiskeli, riadha, Karata Draft   yameanza  October 2 yanaendelea katika viwanja mbalimbali jijini Tanga huku ukitarajiwa kuhitimishwa October 15 yakibebwa na kauli mbiu isemayo 'mazoezi mahala pa kazi huondoa magonjwa yasiyoambukiza.

Share To:

Post A Comment: