Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Samia Suluhu Hassan amezindua Skimu ya Maji ya Kakonko-Kiziguzigu inayotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini [RUWASA] kwa kushirikiana na Taasisi ya Enabel kutoka nchini Ubelgiji. Skimu hiyo inatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi  Bilioni 4 na inatarajiwa kunufaisha kata Nne za Kakonko Mjini, Kiziguzigu, Kasuga na Kanyonza zenye jumla ya vijiji 14.


Akizungumza na watumishi wa RUWASA mara baada ya uzinduzi huo Mheshimiwa Samia amewapongeza watumishi wote wa Wizara ya Maji kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji. Amesema mabadiliko chanya yanayoonekana kupitia wizara hiyo yanatoa matumaini kuwa serikali itafikia malengo yaliyokusudiwa katika sekta ya maji.


“Zamani huko nilikuwa na ugomvi na watu wa maji. Kwa sasa watu wa maji  ni marafiki zangu kweli kweli. Wizara imebadilika. Taasisi zilizoko chini ya wizara zimebadilika. Kazi inafanywa kwelikweli Naomba muendelee hivyohivyo. Amesema Rais Samia. 


Awali akimkaribisha Mhe. Rais Kuzindua mradi huo, Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb)  amesema Mradi wa Kakonko-Kiziguzigu utakapokamilika katika vijiji vyote 14 utahudumia wakazi wapatao 65,010. Nia ni kufikia wakazi wapatao 132,425 ifikapo mwaka 2042 ambao ndio kipindi cha usanifu wa mradi.


Awamu ya kwanza ya mradi imekamilika katika vijiji vya Kakonko, Itumbiko, Mbizi, Kiziguzigu, Kiyobera, Ruyenzi, Kabingo na Kasuga ambapo kwa sasa wananchi wanapata huduma ya maji.


Aidha mradi huo umeongeza hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 51 hadi zaidi ya asilimia 70 huku mgao wa maji ukipungua kutoka saa 5 hadi saa 12 kwa siku. Amesema mipango inaendelea ikiwemo kupanua mradi huo ilii huduma ya maji katika wilaya hiyo ifikie asilimia mia moja.

Share To:

Post A Comment: