Mabadiliko ya Tabia  ya nchi yanasababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu pamoja na hali ya hewa kubadilika na viwango vya joto kuongezeka katika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo nchi ya Tanzania.

Mabadaliko hayo ya tabia nchi yanayosababishwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za kibinadamu ambapo  mataifa makubwa Duniani yakiweka mikakati ya kusaidia nchi za Afrika.


Kwa Tanzania, Serikali imefanya jitihada kubwa za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuandaa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021, Mpango kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2023) na Miongozo na Kanuni za Biashara ya Kaboni, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi. 

Licha ya jitihada hizo za Serikali hali ni tofauti kwa Wilaya ya Longido iliopo  Mkoani Arusha ambapo wananchi wa wilaya hiyo asilimia kubwa ni wafugaji ambao wanakabiliwa na adha kubwa ya ukame uliosababishwa na mabadiliko ya Tabia nchi ambayo yanaathiri nyanda za malisho pamoja na malambo ya kunyweshea mifugo maji.

Mifugo ya wafugaji katika wilaya hiyo imeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kukosa malisho ya uhakika hali inayosababisha mifugo kukonda, kupata magonjwa nyemelezi na kusababisha soko la mifugo kushuka kwa kiwango kikubwa.

Naomi Marko ni Mkazi wa Kijiji cha Ranch Wilayani humo anasema kiangazi sasa kimezidi sana na kimeathiri maisha yao kwa sababu walikuwa wanategemea mifugo na kupata mahitaji ya kujikimu lakini kutokana na mifugo kutokuwa na afya nzuri kwa malisho ya uhakika yanayosababishwa na ukame unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi wanalazimika kutumia muda mwingi kuangalia mifugo hiyo.

"Imebidi nihamishe baadhi ya mifugo yangu kwenda Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara na West Kilimanjaro kutokana na kukosa maeneo ya malisho ya uhakika lakini mbuzi na kondoo wanaweza sana kuvumilia ukame kwa sababu wanakula majani ya juu ya vichaka vidogovidogo lakini kwa ngombe ni vigumu. Hali imekuwa mbaya sana kuna muda mwingine napeleka mifugo kunywa maji  nakosa hata hayo maji mifugo inarudi bila kunywa maji" Alisema

Naomi anatumia fursa hiyo kuiomba serikali kutoa elimu ya upandaji miti kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo inasababisha athari kubwa kwa wafugaji ambao hawana kipato kingine wanachokitegemea zaidi ya mifugo.

"Sisi wafugaji asilimia kubwa hatujabahatika kusoma lakini tukipewa elimu tunaelimika.Nina iomba serikali ya Wilaya ya Longido itoe elimu na kufanya kampeni ya kila mwananchi kupanda miti kwenye maeneo wanayoishi wakati wa kipindi cha mvua ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaathiri mifugo yetu"


David Laizer ambaye pia ni Mkazi wa Kijiji cha Orubomba anayemiliki ng'ombe 100,mbuzi 200 na kondoo 150 anasema kwa kweli mifugo yake inapitia kipindi kigumu sana maana maji yenyewe anapata kwa shida inabidi watoto wawahi kuamka na kutoa mifugo mapema kuipeleka kwenye malisho kwa sababu wanakokwenda kutafuta malisho ni mbali sana kwani muda mwingine wanalazimika kulala huko malishoni.

"Kwa kweli kwa sasa tupo katikati ya moto mkubwa mifugo inakufa sana maji ya kunywesha mifugo tunakosa kabisa na gunia la pumba limekuwa ghali siku baada ya siku mifugo inateseka sana tunaomba serikali ituangalie mabadiliko ya tabia ya nchi yametuhadhiri kwa kiasi kikubwa haswa sisi jamii ya kifugaji"

"Napenda kuiomba serikali yetu iangalie namna gani ya kutujengea malambo ya mifugo yetu na skimu za kunyweshea ngombe maji kwa kuwa mifugo yetu inakufa sana kwa kukosa maji"

Naye Afisa Ustawi wa Jamii Longido Bi. Atuganile Chisunga ameelezea kuwa mabadiliko ya tabia nchi yameweza kuwaadhirikwa kiasi kikubwa wilayani humo kwani ukame umezidi kuwa mkubwa mno na kwamba eneo kubwa la wilaya hiyo ni nyanda za malisho huku eneo dogo sana likibaki  kwa ajili ya kwa kilimo.

"Hivyo basi jamii inahama sana hususani wakina baba na vijana wanahamisha mifugo na kuwaacha wakina mama na watoto wakihangaika wenyewe kujitafutia chakula na mahitaji muhimu ya binadamu,unaweza kuona kwa kiasi gani watoto pia wameadhirika na ukame huu kwa kupata utapiamlo,kwani maziwa waliyokuwa wanategemea kwa sasa nayo hakuna"

"Hususani kwenye swala la Afya nalo limeadhiri sana kwani wakina mama wanaokuja kujifungua wanakuja na afya duni na kusababisha watoto kuzaliwa wakiwa wadogo na kilo moja hadi gramu 800.Sisi sote ni mashahidi tuna matatazo makubwa ya ukame jua linawaka sana, joto kali, mvua hazinyeshi hizi ni athari za mabadiliko ya tabia nchi hivyo tunaendelea na jitihada za kupambana na changamoto hizi.” Alisema na kuongeza

Alisema lazima wao kama serikali wafanye jitihada za kipekee kuwahamasisha wananchi wanapoona ukame waanze kupunguza mifugo yao ili waweze kubakiwa na mifugo michache wanayoweza kuimudu.

Share To:

Post A Comment: